TASAF yajivunia kufikia malengo kwa kaya maskini
Na MWANDISHI WETU
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Zanzibar, umesema umefanikiwa
malengo yake kwa kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo ya kila siku,
zikiwemo katika sekta ya elimu, afya, maji na kuzisimamia kaya zao.
Akizungumzia kuhusu mafanikio ya mpango wa kunusuru kaya masikini
Zanzibar, Mratibu wa Tasaf Zanzibar, Makame Ali Haji, alisema mpango
huo umetekelezwa kwa vipindi vinne kwa mafanikio makubwa.
Alisema Tasaf imetekeleza katika usambaji wa fedha, miradi ya ujenzi
katika maeneo yenye uhitaji, utekelezaji wa miradi ya ajira za muda na
kukuza uchumi wa kaya na kuweka akiba.
Makame alisema kuhusu usambazaji wa fedha kwa upande wa Zanzibar,
zaidi ya kaya 54,425 zimewezeshwa na zaidi ya Sh, bilioni 52
zimetumika.
"Fedha hizo zimewawezesha wananchi kuanzisha miradi midogo midogo ya
kuzisaidia kaya zao na kuhakikisha wanakuza vipato vyao, makazi yao
pamoja na kuendelea maisha yao", amesema.
Kupitia utekelezaji wa ajira za muda, Tasaf imetekeleza zaidi ya
miradi 711 kwa upande wa Unguja na Pemba, katika sekta ya misitu,
maji, afya, elimu na ukarabati wa barabara za ndani ili wananchi
wapate huduma kukuza uchumi wa kaya zao.
"Miradi hii 711 imesaidia sana kutatua changamoto mbalimbali kaya na
kuwainua kiuchumi wananchi kwa ujumla", amesema.
Kipengele cha ujenzi wa miundombinu, Makame alisema Tasaf kupitia
miradi katika sekta ya afya na elimu, ambapo zaidi ya Sh. bilioni 4,
zimetumika katika sekta hizo.
Makame amesema kupitia mpango wa Tasaf wametekeleza ujenzi wa
madarasa, ukarabati wa barabara na ujenzi wa vituo vya afya katika
maeneo yenye uhitaji.
Kupitia miradi ya uwezeshaji jamii kiuchumi, Makame amesema baada wa
wanufaika kupatiwa fedha kupitia usambazaji, kuna ruzuku maalumu
zimetolewa kwa kaya 24,435 Unguja na Pemba.
Amesema katika utekelezaji huo zaidi ya Sh. bilioni 9.4 zimetmika
kuwawezesha kupitia miradi midogo midogo, ikiwemo kuanzisha miradi ya
ufugaji, kilimo, biashara ndogo na huduma, ambapo wananchi wengi
wamepiga hatua na kupelekea kutoa ajira kwa wengine.
"Mengi yamefanyika katika muungano huu ambao umefika miaka 61,
naishukuru serikali na wananchi kwa kuhakikisha kila kinachopangwa
kinafikia malengo, ambapo mpango wa kunusuru kaya masikini
umefanikiwa", amesema.
Kwa upande wa wanufaika wa TASAF wamesema mpango huo umewasaidia
kutimiza ndoto zao katika sekta ya elimu, ujasiriamali na kuwainua
kiuchumi.
Mwanafunzi wa Chuo cha Abdulrahman Al-Sumaiti, Miraji Alfani Musa,
amesema TASAF imekujua kuinua familia za watu wa chini, imemsaidia
tangu akiwa kidato cha nne hadi sasa kupitia kwa wanufaika wazazi
wake.
"Nimepata mkopo wa elimu ya juu kutoka Bodi ya Mikopo, kwa msaada
TASAF nilipewa kipaumbele, hivyo naishukuru serikali kwa kuwa na
mpango huu muhimu kwa wenye kuhitaji, naomba Tasaf iwe endelevu",
amesema.
Naye mwanafunzi wa Chuo Kikuu Zanzibar (SUZA), Mtumwa Ali Haji,
amesema alifurahi kufaulu kwa kupata ufaulu wa daraja la pili kidato
cha nne, lakini wazazi wake walimwambia hawana uwezo wa kumuendeleza
ndipo alikata tamaa ya kutimiza ndoto zake.
Mtumwa amesema furaha yake ilirejea baada wazazi kufikiwa kwa kujiunga
mpango wa TASAF, ambapo alipatiwa mkopo wa elimu kutoka bodi ya mikopo
na kuendela na masomo, ambapo anasoma Shahada ya Manzingira kataika
chuo hicho.
"TASAF ndoto yangu ni kuwa waziri wa mazingira, sasa matumaini hii
ndoto itatimia kupitia fursa hii Tasaf", mesema.
Mkazi wa Kiembe Samaki, Hamid Juma Sheha, amesema alikuwa katika
mpango huo, alianza kulipwa kidogo kidogo baada muda akupita alipewa
fedha nyingi, akaamua kuanzisha miradi mbalimbali ya kumuendeleza.
"Nilipopata fungu kubwa Sh. 450,000 kutoka TASAF nikaanza kukusanya
malighafi na kumchukua kijana wa kunisaidia katika kazi yangu ya
kutengeneza chaga za udogo za kutengeneza majiko, baada kupata faida
nikaanzisha mradi mwingine wa kuku, nilianza na kuku 100 na sasa nina
kuku 300", amesema.
Hamid amesema kupitia TASAF amefanikiwa kupata fedha kusomesha watoto
wake wawili katika ngzi chuo na wengine wawili wako kataika shule za
msingi.
Pia Hamid ameshukuru mpango huo kwa kumuinua kiuchumi, amewashauri
wanufaika wengine kujifunza kwake kwa kutumia fedha wanazopewa
kuanzisha miradi kuliko yote kuingiza katika matumizi tofauti.
Reviewed by Gude Media
on
April 26, 2025
Rating:



