Jaji Mutungi ahimiza amani na mshikamano kuelekea Uchaguzi Mkuu
Na MWANDISHI WETU
Msajili wa Vyama Vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amewataka viongozi wa vyama vya siasa kuwahimiza wananchi wakiwemo wanachama wao, kufuata sheria kudumisha amani na mshikamo hususan kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Mutungi amesema hayo jijini Dar es Salaam jana, katika kikao maalumu na wahariri wa vyombo vya habari kujadili masuala tofauti ikiwemo maandalizi ya uchaguzi.
“Ni vyema tukawa makini kipindi hiki hususan viongozi wa vyama vya siasa, wajue kuwa uchaguzi utapita maisha yataendelea, tudumishe amani na mshikano kwani ndiyo msingi wa maendeleo,”alisema.
Mutungi amesema kuelekea uchaguzi mkuu kunakuwa na matukio mengi na ongezeko la joto la uchaguzi katika nchi zote, ni vyema kuwa makini kuhakikisha kuwa demokrasia inadumishwa.
“Katika kipindi kama hiki, habari za uongo huwa zinaongezeka, yaani habari zisizo na vyanzo halisi, mfano ni ule waraka wa TEC, ulioghushiwa, ni vyema wananchi wakatafuta taarifa katika vyanzo rasmi vinavyoaminika,”alisema.
Aidha Mtungi amesema sasa wameanza utaratibu wa kuvijengea uwezo vyama vya siasa katika masuala ya uchaguzi mkuu, ambapo walianza Zanzibar na wataendelea Dar es Salaam, lengo ikiwa ni kuhakikisha kuwa vyama vinapata maarifa ya kutosha kushiriki uchaguzi kwa amani na mshikamano.
Amesema wataendelea kushirikiana na vyombo vya habari na watatoa mafunzo kuelekea uchaguzi mkuu kuwajengea uwezo kwa namna njema ya kutekeleza majukumu yao.
Reviewed by Gude Media
on
May 03, 2025
Rating:


