Tume ya TEHAMA, THN wakubaliana kuimarisha vituo vya ubunifu
Na Mwandishi Wetu
Tume ya TEHAMA na Mtandao wa Vituo vya Ubunifu Tanzania (THN) wamesaini makubaliano ya kushirikiana katika kujenga uwezo wa vituo hivyo ili viweze kuleta tija kwa wabunifu kote nchini na kuinua uchumi.
Kusainiwa kwa makubaliano hayo kati ya Tume na THN yenye vituo takribani 50 katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani, ni matunda ya Tume ya TEHAMA katika kutimiza jukumu lake la kuratibu na kuhamasisha ukuaji na matumizi ya TEHAMA nchini, hasa katika eneo la ubunifu.
Eneo hilo la ubunifu lina vijana wengi wajasiriamali ambao kama wataandaliwa vyema na kuwa na mang'amuzi stahiki kupitia ubunifu wao wataleta msukumo mkubwa kuelekea katika uchumi wa kidijitali.
Akizungumza wakati wa kusainiwa kwa makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume, Dkt. Nkundwe Mwasaga aliishuruku THN kwa kuamua kufanya kazi na Tume ya TEHAMA hivyo kuhamasisha na kutambua mchango wa bunifu mbalimbali katika ukuaji wa Uchumi wa kidijitali.
“Hii ni hatua ya kimkakati katika kuhakikisha kuwa bunifu zinazotokana na vituo vya ndani zinapata mazingira wezeshi ya kustawi, kuungwa mkono na hatimaye kuwa suluhisho kwa changamoto za kijamii na kiuchumi. " alisema Dkt. Nkundwe na kuongeza kuwa Tume itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha hakuna mbunifu anayeachwa nyuma katika safari ya kidijitali
Makubaliano haya yanakuja katika wakati ambapo Serikali imeweka mkazo katika kukuza uchumi wa kidijitali, na kuweka mazingira wezeshi kwa vijana, wabunifu na wajasiriamali kutumia TEHAMA kama kichocheo cha maendeleo. Kupitia ushirikiano huu, Tume ya TEHAMA itaimarisha nafasi yake kama msimamizi mkuu wa sera, uratibu na uhamasishaji wa matumizi ya TEHAMA nchini kwa kuwa karibu zaidi na jamii ya wabunifu.
Naye Mwenyekiti Mtandaji wa THN, Kiko Kiwanga alisema makubaliano hayo yatauwezesha mtandao wao kushirikiana kwa karibu na Serikali kung’amua na kutatua changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa kikwazo kwa vijana na wajasiriamali kuibua fursa za kiuchumi kupitia TEHAMA.
Aidha, makubaliano haya yataiwezesha THN kutangaza mafanikio na bunifu mbalimbali kupitia majukwaa ya kiserikali na yenye mahusiano na serikali na hivyo kupanua wigo wa fursa za kiuchumi kwa wabunifu na wajasiriamali katika TEHAMA.
“Huu ni mwanzo wa ukurasa mpya kwa wabunifu nchini. Tunafurahia kushirikiana na Tume ya TEHAMA ili kuibua fursa mpya, kushirikisha Serikali kwenye utatuzi wa changamoto, na kuhakikisha ubunifu unakuwa chachu ya maendeleo.” alisema.
Kupitia makubaliano hayo, Tume ya TEHAMA ICTC na THN wataendesha kwa pamoja shughuli mbalimbali za mafunzo, midahalo ya kitaalamu, tafiti, na programu za kukuza ujuzi wa TEHAMA katika vituo vya ubunifu. Aidha, ushirikiano huu unalenga kuhamasisha usawa wa kijinsia na ushirikishwaji wa makundi maalumu kama wanawake na vijana katika sekta ya TEHAMA.
Reviewed by Gude Media
on
June 19, 2025
Rating:


