Wanaushirika washauriwa kutumia hisa kwa uwekezaji
Na MWANDISHI WETU
Vyama vya Ushirika vimeshauriwa kutumia hisa za Chama cha Ushirika katika kuongeza thamani ya Ushirika hasa kwa kupitia Uwekezaji unaoongeza mapato na tija kwa Wanaushirika na kukuza Vyama.
Amesema hayo Afisa Ushirika Mwandamizi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Ndimolwo Laizer akitoa mafunzo ya kuwajengea uwezo Wakulima wa mazao ya bustani wa Halmashauri ya Mji Tunduma Mkoani Songwe Juni 9, 2025.
Amesema hisa Wanaushirika ni vyema zitumike kwa kuwekezwa kwa ridhaa ya Wanachama kupitia Mikutano mikuu kuongeza mnyororo wa thamani ya uzalishaji kama vile kununua mashine za kuongeza thamani ili kuongeza mapato zaidi ya Chama kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Miongozo ya Ushirika.
Afisa Ushirika Bi. Flora Daud nae akitoa mada katika mafunzo hayo ameshauri Vyama vya Ushirika kuzingatia misingi ya ushirika, mgawanyo wa uongozi katika vyama vya Usirika, Ushirika kujiendesha kibiashara na kutumia njia za kidijitali kujitangaza ili kuongeza wigo wa masoko ya mazao ndani na nje ya nchi.
Mada nyingine zilizofundishwa katika mafunzo hayo ni pamoja na dhana ya TANSHEP ambayo humtaka mkulima kuanzia sokoni na kumalizia shambani kwa kipato zaidi, Kanuni za kilimo bora cha mazao ya Bustani pamoja na Sera za Serikali juu ya Kilimo cha mazao ya Bustani.
Mazao ya bustani yanayozalishwa na Vyama vya Ushirika ni pamoja na viungo, mbogamboga, maua, matunda katika maeneo mbalimbali.
Reviewed by Gude Media
on
June 10, 2025
Rating:
