Rais Dk. Samia mgeni rasmi Tuzo za Kimataifa za kuhifadhi Quraan

Na MWANDISHI WETU

RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Tuzo za za Kimataifa za Kuhifadhi Quraan Tukufu Aprili 23, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Aidha Taifa la Saudi Arabia, limetangaza neema katika mashindano hayo ikiwa ni pamoja na kumleta mmoja wa maimamu wakubwa wa msikiti mtakatifu wa Macca nchini humo na kutoa tiketi za hija kwa wananchi watano waakaohudhuria mashindano hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Taasisi ya Kuhifadhisha Quraan Tanzania ambao ni wandaaji wa tukio hilo, Sheikh Othuman Kapolo, amesema washiriki wa  mashindano hayo ni 25 kutoka mabara yote matano duniani.

Amesema licha ya tiketi hizo za hija pia watatoa zawadi mbalimbali kwa wananchi watakaohudhuria zikiwemo simu na pikipiki, hivyo kuwahimiza wananchi kuhudhuria kwa wingi kwani hakutakuwa na kiingilio.

Balozi wa Saudi Arabia hapa nchini , Yahya Ahmed Okeish, amesema tuzo za kimataifa za Quraan tukufu ni mbegu iliyopandwa na imechipua kwa watanzania.

 Tuzo hizo zimezinduliwa leo na Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Mkuranga, mkoani Pwani, Abdallah Ulega ambaye amesema ujumbe wa tuzo hizo unaosema Quraan ni amani umekuja wakati muafaka ambapo Tanzania inaelekea kufanya uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu, hivyo suala la amani ni muhimu.