Serikali yapongezwa jitihada za maboresho ya sheria nyongeza siku za likizo wanaojifungua watoto njiti

Na MWANDISHI WETU

WADAU mbalimbali wa Kazi na Afya, wamepongeza jitihada za serikali kupitia Wizara ya Afya, za kufanyia kazi maboresho ya sheria ya wafanyakazi wanaojifungua watoto njiti kuongezwa siku za likizo kuimarisha afya ya mzazi na mtoto.

Wakizungumza, baada ya kuwasilisha maoni hayo katika kikao cha kamati ya Kudumu ya Bunge, ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, kuhusu muswada wa sheria ya maendeleo, marekebisho ya sheria za kazi za mwaka 2024, walipongeza jitihada hizo za serikali kufanyia kazi jambo linalojali afya ya mama na mtoto.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Doris Mollel, amesema serikali ya Rais Dk. Samia ni sikivu, hivyo wanafurahi kuona maoni yao yamepokelewa na kamati husika kwa lengo la kulifanyia kazi muswada wa nyongeza ya siku za likizo hususan kwa wamama wanaojifungua watoto njiti. 

“Tunaishukuru serikali, kupitia wizara ya afya kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea kuifanya, kufikia hatua hii ya kukusanya maoni ya muswada huo, ni hatua kubwa ambayo tunaamini itazaa matunda ya sheria mpya yenye nyongeza ya siku.

“Nimefurahi kuwasilisha Muswada wa Sheria ya marekebisho ya sheria za Kazi, Bungeni Dodoma. Nimetumia kikao hicho kuwahabarisha wajumbe jitihada zinazofanywa na serikali kutatua changamoto zinazowakabiri Watumishi Tanzania wakiwemo wale wanaojifungua watoto njiti na changamoto za utatuzi wa migogoro ya Ajira Nchini,”amesema.

Amewapongeza wadau mbalimbali wa afya na wafanya kazi ikiwemo vyama vya wafanya kazi, kwa kazi kubwa ambayo wameendelea kuifanya ya kutoa maoni mbele ya kamati hiyo kuhusu umuhimu wa maboresho hayo ya nyongeza za siku.

 Katibu Mkuu wa TUGHE ambaye pia ni Katibu Mkuu wa TUCTA, Hery Mkunda ameushukuru Uongozi wa Bunge kwa kutoa nafasi kwa Vyama vya Wafanyakazi, ambao ni wadau muhimu wa masuala ya kazi kutoa maoni na mapendekezo kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Kazi wa Mwaka 2024.