DC Kahama ajivunia matunda ya kodi wilayani kwake
Na MWANDISHI WETU
Mkuu wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Mboni Mhita, amewataka wananchi kuendelea kulipa kodi na kujivunia maendeleo yanayopatikana kutokana na kodi wanazolipa.
Mboni ameyasema hayo leo Machi 18, 2025 alipokutana na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), waliofika ofisini kwake kujitambulisha katika kampeni ya elimu ya kodi ya mlango kwa mlango inayoendelea wilayani humo.
Amesema ndani ya Wilaya kuna miradi ambayo inatokana na kodi wanazolipa wananchi.
"Kodi tunalipa ndiyo zinatumika na serikali kufanya maandaleo haya katika jamii, sisi wa Kahama tunajivunia hospitali ya kisasa inayofanana na kanda, ukiangalia zahanati za kisasa katika wilaya yetu", amesema.
Kwa upande wake, Ofisa Mkuu Msimamizi wa kodi TRA, Lameck Ndinda, amesema lengo la kampeni hiyo ni kutoa elimu ya kodi na kusikiliza changamoto na maoni ya wafanyabiashara ili kuweza kuboresha huduma zao
Ndinda amesema wamebaini kuna baadhi ya wafanyabiashara bado hawajakadiriwa na na wengine kutokutoa risiti vizuri.
Aidha, Ndiba ametoa wito kwa wafanyabiashara kwenda kukadiriwa kabla ya tarehe 31 Machi ili kuepuka adhabu.
"Wito wangu kwa wafanyabiashara kujitokeza kwa wingi kwenda kukadiriwa kabla ya tarehe 31 mwezi Machi, na wakisha kukadiriwa wawahi kufanya malipo ya awamu ya kwanza", amesema.
Naye, mmoja wa wafanyabiashara, Tumaini Kinanda, amesema kampeni hiyo inasaidia kuboresha uhusiano kati ya TRA na wafanyabiashara.
Kinanda ameomba kampeni hiyo iwe endelevu waweze kujifunza zaidi mambo mbambali ya kodi.
.jpeg)