Diwani Dotto akabidhi gari la wagonjwa na X Ray Kituo cha Afya Kata ya Kigamboni, amshukuru Rais Dk. samia
Na MWANDISHI WETU
Diwani wa Kata ya Kigamboni, Dotto Msawa, amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwashushia neema ya fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika kata hiyo.
Dotto ametoa shukrani hizo, Kigamboni, Da r es Salaam, baada ya kukabidhi gari jipya la kubebea wagonjwa lenye thamani ya Sh. Milioni 205 na mashine mpya ya X-Ray yenye thamani ya Sh. Milioni 199,864,000.
"Namshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo amekuwa akiguswa na changamoto zinazowakabili wananchi wa Kata ya Kigamboni na kuwashushia fedha nyingi za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya Kata ya Kigamboni", amesema.
Dotto amesema kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dk. Samia, Kata ya Kigamboni imenufaika na miradi mingi ikiwemo ujenzi wa barabara mpya za lami katika mitaa ya Kigamboni kupitia mradi wa DMDP awamu ya pili ambapo kata ya hiyo imepata kilometa 10 na sasa wakandarasi wapo kazini kuendelea na ujenzi.
Amesema katika sekta ya elimu kata hiyo imenufaika kupata Shule ya Sekondari ya Ghorofa Paul Makonda, kupitia mradi wa booster, madarasa mapya na ukarabati wa madarasa ya zamani katika shule za msingi zilizopo ndani ya Kata ya Kigamboni
"Kwa upande wa sekta ya Afya mbali na gari la kubebea wagonjwa sambamba na mashine ya X-ray vilivyokabidhiwa leo, pia ndani ya miaka minne ya uongozi wa Dk. Samia tumepata jengo jipya la huduma ya mama na mtoto na uboreshaji wa huduma za afya, ikiwa ni upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa, ongezeko la madaktari na wauguzi na upatikanaji wa dawa za kutosha katika kituo cha Afya Kigamboni.
Pia, kata hiyo imenufaika kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu kupata mikopo ya asilimia 10 kutoka Halmashauri, pia zaidi ya vijana 100 wamepata mafunzo ya ufundi kutoka Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) kupitia jukwaa la uwezeshaji vijana kiuchumi inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana Ajira na Watu Wenye Ulemavu.
Dotto amesema katika kipindi cha miaka minne ya Dk. Samia, upatikanaji wa huduma za umeme na maji safi na salaama umeimarika katika kata hiyo.
