Kamati ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI yaipongeza Barrick Bulyanhulu utekelezaji kanuni za afya
Na Mwandishi Wetu
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, imeridhishwa na utekelezaji wa programu za afya, ndani na nje ya Mgodi wa Barrick Bulyanhulu za kupambana na magonjwa kwa wafanyakazi na wananchi wanaoishi katika vijiji vinavyozunguka mgodi huo, mkoani Shinyanga.
Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Hassan Mtenga, akizungumza baada ya kukagua mgodi huo, juzi, wilayani Kahama, alisema programu hiyo imetekelezwa kwa ufanisi katika kupambana na magonjwa yakiwemo, UKIMWI, Malaria, Kifua Kikuu na magonjwa mengineyo yanayoweza kusababishwa na shughuli za uzalishaji mgodini.
"katika wasilisho lenu tumeona ni jinsi gani kampuni iko mstari wa mbele kulinda afya za wafanyakazi wake na jamii nzima ya maeneo yanayozunguka mgodi na kwa jinsi inavyofanikisha miradi ya Afya kupitia fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), pia tumefurahi kusikia asilimia kubwa vya wafanyakazi katika migodi ya Barrick hapa nchini ni Watanzania", alisema.
Pia Mtenga alitoa pendekezo kwa mgodi wa Barrick kuangalia uwezekano wa kuchangia katika Mfuko wa Taifa wa UKIMWI, kwa kushirikiana na Serikali ya mkoa na wilaya kupitia kamati za naendeleo ya jamii.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Madini, Dk.Steven Kiruswa, alisema uendeshwaji wa migodi ya Barrick ambayo ina ubia na Serikali kupitia Kampuni ya Twiga Minerals ni wa weledi mkubwa na viwango vya kimataifa.
Amesema ubia huo baina ya serikali umekuwa wa uwazi, unazingatia sheria za nchi na ni kielelezo cha uwekezaji wa kupigiwa mfano katika sekta ya Madini nchini.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, amepongeza mgodi huo kwa kuhakikisha unafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na Serikali kwa kufanikisha miradi mikubwa ya maendeleo katika mkoa hususani sekta za elimu, Afya, Maji na ujenzi wa miundo mbinu ya barabara.
Kwa upande wa Meneja Mkuu wa Mgodi, Victor Lule, amesema mgodi uko mstari wa mbele kuendesha programu za kudhibiti maambukizi ya UKIMWI na Malaria kwa wafanyakazi wake pia umeimarisha Zahanati ya mgodi kuhakikisha wanatoa huduma bora za kisasa kwa Watanzania.
Lule wameboresha Kituo cha Afya cha Bugarama na kupeleka kampeni ya kupambana na Malaria ijulikanayo 'Zero Malaria', katika vijiji vinavyozunguka mgodi kwa kupuliza dawa za kuua mazalia ya mbu na kugawa wananchi vyandarua vyenye dawa.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TACAIDS, Dk. Catherine Joachim , ameshauri mgodi huo kuendesha programu za tohara kwa wanaume na dawa za kuzuia maambukizi mapya ndani na nje ya mgodi.
Amesema licha ya kuwepo dawa za kufubaza makali ya virusi vya UKIMWI, bado kuna maambukizi mapya yanaendelea kujitokeza na sehemu mojawapo hatarishi kupata ugomjwa huo ni maeneo ya migodini.
Kwa mujibu wa utafiti wa mwaka jana, takwimu zinaonyesha watu milioni 1.7 wanaishi na virusi vya ukimwi nchini wakati mwaka 2022/23 utafiti ulionyesha watu 60,000 waliambukizwa virusi vya ukimwi ambapo sehemu za migodini. zinatambulika kama sehemu hatarishi.
