Mavunde awataka wakazi wa Dodoma kuchagua nishati safi kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi
Na MWANDISHI WETU
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amewataka wakazi wa Dodoma kuunga mkono juhudi za serikali kwa kuchagua nishati safi ya kupikia kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Akizungumza katika uzinduzi wa PumaGas, juzi, jijini humo, Mavunde alisema upatikanaji wa huduma ya nishati safi nchi nzima na kuhakikisha ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.
Alisema Uwekezaji huo kupitia bidhaa ya PumaGas utakuwa chachu ya kuwapatia wananchi chaguo rahisi na la uhakika la nishati kwa matumizi ya nyumbani na kibiashara.
"Niwapongeze Kampuni ya Puma Energy Tanzania kwa kushirikiana na serikali kuunga mkono jitihada za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha ifikapo 2030, asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia", alisema.
Mavunde alisema ushirikiano kati ya sekta za umma na binafsi ni muhimu katika kufanikisha malengo ya kitaifa ya kukuza matumizi na kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi, hususani kwa maeneo ya vijijini ambayo bado upatikanaji wake unakumbana na changamoto mbalimbali.
Pia Mavunde alisema kiwango cha matumizi ya nishati safi nchini bado hakiridhishi na kinaathiri taifa kwa kiasi kikubwa hususan kimazingira na kiafya, bado Watanzania wanategemea kuni na mkaa kupikia, ingawa rasilimali za nchi zinatosheleza kuwafanya waachane na mazoea haya.
"Ninawaomba pia uzinduaji wa huduma hii uendane na shughuli za utoaji elimu na uhamasishaji kwasababu bado watu wengi wanadhahania kuwa nishati safi ya kupikia ni gharama na siyo salama. Serikali tuko nanyi bega kwa bega kuhakikisha mnalifanikisha hili na kuwafikia wananchi wengi zaidi hususani maeneo ya vijijini,” alisema.
Pia kampuni hiyo ilikabidhi mitungi msaada wa mitungi ya gesi kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi na Mbunge wa Chamwino, Deogratius Ndejembi.
Ndejembi alisema msaada huu utayanufaisha makundi mbalimbali ya jamii wilayani Chamwino katika kuboresha shughuli za kijamii na kiuchumi.
"Nawaomba wadau wengine pia kupanua uwekezaji wao katika miundombinu na minyororo ya usambazaji ili kuhakikisha kuwa suluhisho la nishati safi linafikia kote nchi. Tunatambua kwamba ufikiaji wa nishati safi bado ni changamoto, hususan katika jamii za vijijini na zisizofikika kiurahisi.
Pia Ndejembi alitoa wito kwa watu wote kuwa mabalozi wa mabadiliko, kuwahamasisha na kuwaelemisha watu wengine kuanza kutumia nishati safi kwa maendeleo endelevu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Fatma Abdallah, alisema wamejizatiti katika uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya uhifadhi, maeneo ya manunuzi na mawakala wa usambazaji wa mitungi ya gesi.
Alisema dhamira ya kampuni hiyo ni kuunga mkono serikali kufikia lengo lake la mabadiliko ya suluhisho la nishati endelevu ambayo inaboresha afya ya umma na ustawi wa kiuchumi kwa kizazi cha sasa na kijacho.
" Mkakati wa upikaji safi wa Tanzania unalenga kufikia asilimia 80 ya watu kuhamia kwenye upikaji safi na kutoa wito kwa sekta binafsi kuongeza uwekezaji katika gesi safi asilia. Gesi safi asilia ni njia salama, rahisi na ya gharama nafuu ya kuzipa jamii zetu nishati, kuwezesha upikaji safi na kupunguza madhara yanayotokana na matumizi ya nishati asilia za kupikia", alisema.
