Mitawi azikumbusha wizara kufungamanisha taarifa za mazingira
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Hayo yamesemwa Machi 20, 2025, jijini Dodoma na Naibu
Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais, Abdallah Hassan Mitawi, akifungua kikao kazi cha
kukuza uelewa kwa wadau wa Wizara za kisekta kuhusu uandaaji wa mfumo jumuishi
wa usimamizi wa mazingira nchini.
Mitawi amesema mazingira ni sekta
mtambuka inayogusa Wizara zote za kisekta ndani ya Serikali na hivyo upo umuhimu wa kuandaa mfumo jumuishi
utakaorahisisha upatikanaji wa taarifa zitakazosaidia taifa kubaini changamoto
za mazingira na kuzipatia ufumbuzi wa pamoja.
“Sote ni mashahidi kuhusu athari za
mabadiliko ya tabianchi zilizopo kwa sasa duniani na Tanzania kwa ujumla ambazo
zimegusa sekta zote muhimu za kiuchumi ikiwemo kilimo, mifugo, uvuvi, fedha
n.k...hivyo hatuna budi kuimarisha ushirikiano” amesema Mitawi.
Aidha Mitawi amesema Serikali kupitia
Ofisi ya Makamu wa Rais imekusudua kuanzisha mfumo huo wa ukusanyaji wa taarifa
za mazingira ikiwa ni hatua muhimu ya kurahisisha na kuimarisha sekta ya hifadhi
ya mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Ameongeza kuwa Wizara za kisekta
zimekuwa zikitekeleza majukumu mbalimbali kuhusu uhifadhi wa mazingira lakini zimeshindwa
kuwa na mfumo wa utambuzi na kusababisha ukosefu wa taarifa na muhimu pindi
zinapohitajika kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo.
Amefafanua kuwa kwa mujibu wa Sheria
ya usimamizi wa mazingira Sura 191 kifungu 175 Ofisi ya Makamu wa Rais, imepewa
jukumu la kusimamia mchakato wa ukusanyaji wa taarifa za mazingira nchini
ambazo zimekuwa zikitumika katika majukwaa na mikutano mbalimbali ya kimataifa.
Kwa mujibu wa Mitawi amesema uandaaji wa
mfumo jumuishi utasaidia kutatua changamoto mbalimbali zilizojitokeza hapo
awali kuhusiana na upatikanaji wa taarifa za mazingira, na hivyo kuzitaka
Wizara za kisekta kutoa ushauri, maoni na mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha
mfumo huo.
Kwa upande Kaimu Mkurugenzi wa
Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Paul Deogratius amesema mfumo huo
umekuja kwa wakati mwafaka kwani utawezesha taarifa mbalimbali za mbalimbali
katika Wizara za kisekta kuweza kusomana na hivyo kusaidia katika mipango ya
maendeleo.
“Mwaka 2022 tulipoandaa Mpango Kabambe
wa Mazingira tulipata taarifa mbalimbali za Wizara za kisekta katika eneo machache
na hivyo kuwepo kwa mfumo huu kutasaidia upatikanaji wa taarifa za mazingira nchini”
amesema Dkt. Paul.
Amesema kuwa Serikali imekuwa ikifanya
kazi nzuri kuhusu masuala ya uhifadhi wa mazingira lakini zimeshindwa kuripotiwa
na kuonekana kutokana na ukosefu wa mfumo sahihi wa utunzaji na uhifadhi wa
taarifa hizo.
Naye Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA, Ofisi
ya Makamu wa Rais Bi. Joyce Mnunguli amesema Ofisi
hiyo imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kukamilisha mfumo huo
ambao utasaidia kujibu changamoto mbalimbali za ukosefu wa taarifa za mazingira
nchini.
“Ofisi inashirikiana na Baraza la
Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na wadau wengine katika
uandaaji wa mfumo na mpaka sasa tumeandaa andiko na tunaendelea na uandaaji na
utayarishaji wa nyaraka mbalimbali zitakazotumika katika mfumo huu” amesema.
