UDOSO yamuunga mkono Rais Dk. Samia kufadhili wanafunzi wanaopitia mazingira magumu UDOM
Na MWANDISHI WETU
Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOSO), yaunga mkono juhudi za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan za kutoa ufadhili kwa Wanafunzi, wanaopitia mazingira magumu ya kulipia ada za masomo, kupitia faida ya uwekezaji wa hati fungani ya Benki Kuu (BOT) iliyonunuliwa tarehe 19 Disemba, 2024.
Hilo limebainishwa na Waziri wa Fedha wa UDOSO, Angelina Abdallah Kilondo, ambapo alisema Serikali ya Wanafunzi imewekeza kiasi cha sh. Milioni Mia Moja na faida yake itatumika kusaidia wanafunzi wenye uhitaji kupitia UDOSO Scholarship Bond.
"Hatua hii ni sehemu ya jitihada za serikali ya wanafunzi kujiongezea kipato kwa njia endelevu ambapo mapato yanayotokana na uwekezaji huu, yatatumika kusaidia wanafunzi wenye uhitaji," alisema.
Naye Makamu wa Rais wa UDOSO, Jacquiline Humbaro amesema, kila mwaka wanafunzi 11 watapata ufadhili huo kwa njia ya ushindani, kama inavyofafanuliwa na Kanuni za Ufadhili kupitia “UDOSO Scholarship Bond” zilizopitishwa katika Mkutano wa 90 wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dodoma wa Machi 6, mwaka huu.
“UDOSO tunatambua jitihada za Serikali ya Awamu ya 6 inayoongozwa na Mama Dk. Samia Suluhu Hassan za kufadhili wanafunzi wa vyuo vikuu kupitia “Samia Scholarship”. Ni kwa muktadha huo, Serikali ya UDOSO 2024/25 imeona umuhimu wa kuunga mkono jitihada za Mama Samia ili kuwezesha wanafunzi wengi zaidi waweze kupata elimu ya juu”. Alimalizia Jacquiline.
Amesema sh.100,000,000 katika hati fungani za BOT kupitia wakala wake ambaye ni Benki ya CRDB katika kipindi cha miaka 20 na utazalisha riba ya wastani wa shilingi milioni kumi na tano kwa riba ya asilimia 15.49 kwa mwaka.
Amesema faida kutokana na uwekezaji huo umepangwa kuwa Sh.15,000,000 kila mwaka kwa miaka yote 20 ya uwekezaji. Matumizi ya faida inayotokana na bondi yatakwenda kusomesha wanafunzi kupitia “UDOSO Scholarship Funda”.
