Yas Tanzania yaandaa futari maalumu kwa wateja Zanzibar
Na MWANDISHI WETU
Kampuni ya Mawasiliano ya Yas Tanzania imefanya hafla maalumu ya futari na wateja wake wa Zanzibar katika Hotel Verde, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku 100 tangu mabadiliko rasmi ya chapa kutoka Tigo, TigoZantel na Tigo Pesa kwenda Yas na Mixx by Yas.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana Mustafa, washirika wa kibiashara, wateja wa Yas & Mixx by Yas na wadau mbalimbali wa sekta ya mawasiliano.
Akizungumza katika hafla hiyo juzi, Mustafa aliipongeza Yas Tanzania kwa mchango wake mkubwa katika kukuza uchumi wa Zanzibar kupitia huduma za mawasiliano pamoja na huduma za kifedha kwa njia ya simu.
Vilevile alitumia fursa hiyo kuishauri Kampuni ya Yas Tanzania kutuma jumbe za kuhamasisha amani kwa wateja wake kwakua mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi.
"Yas Tanzania imeendelea kuonyesha dhamira ya dhati katika kuwahudumia wateja wake na jamii ya Zanzibar kwa ujumla. Hata hivyo, kwa kuwa mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi, naomba kampuni hii itumie majukwaa yake mbalimbali kuhamasisha amani, utulivu, na mshikamano miongoni mwa wananchi," alisema.
Kwa upande wake, Ofisa Mkuu wa Fedha wa Yas Tanzania, Innocent Rwetabura, aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano wake katika kufanikisha mabadiliko ya chapa za Yas na Mixx by Yas, ambayo yameleta mageuzi makubwa kwenye sekta ya mawasiliano nchini.
"Tunaposherehekea siku 100 za Yas na Mixx by Yas, tunajivunia kuwa tumeweza kuwa karibu zaidi na wateja wetu na kuwafungulia fursa nyingi za kidijitali. Katika kipindi hiki kifupi, tumepokea mapokezi chanya kutoka kwa wateja wetu, na tumeendelea kuwekeza katika teknolojia na huduma bora ili kuimarisha zaidi uzoefu wao," alisema Rwetabura.
Katika hotuba yake, Rwetabura alieleza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika siku 100 za Yas na Mixx by Yas, ikiwa ni pamoja na tuzo mbalimbali za umahiri zikiwemo za Ookla na TEHAMA Awards, pamoja na kutambuliwa na TRA kama mlipaji mkubwa wa kodi katika Ushuru wa Forodha.
Ameongeza pia katika ushirikiano wa kimkakati, Yas imeanzisha ubia na taasisi mbalimbali kama Zanzibar Petroleum Limited (ZPL), DSE, na e-Government Agency Zanzibar (EGAZ) ili kuimarisha huduma zake kwa Watanzania.
