Diwani Klerruu: Rais Dk. Samia ameandika historia utekelezaji miradi ya miundombinu Kata ya Mabibo
Na MWANDISHI WETU
Diwani wa Kata ya Mabibo, wilayani Ubungo, mkoani Dar es Salaam, Joseph Klerruu, ameishukuru na kuipongeza serikali chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake kwa utekelezaji miradi ya maendeleo yenye thamani ya Sh. bilioni 15.2 katika kata hiyo.
Klerruu amesema utekelezaji huo wa miradi umevunja rekodi katika kata hiyo tangu Tanzania ilipopata uhuru mwaka 1961, ambapo Sh. 12,315,000,000 kimeelekezwa katika ujenzi, uboreshaji na ukarabati wa miundombinu.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mwaka wa fedha 2020-2025 katika Baraza Maalumu la Umoja wa Vijana wa Chamama Cha Mapinduzi (UVCCM) Kata ya Mabibo, Dar es Salaam, amesema fedha hizo zimetumika katika utekelezaji wa miradi kwa mwaka huo wa fedha, ikihusisha sekta zote zikiwemo za miundombinu, afya, elimu, maendeleo ya jamii, biashara, masoko, ulinzi na usalama, utawala, michezo na utamaduni.
Klerruu amesema miongoni mwa miradi iliyotekelezwa ni ujenzi wa barabara ya lami ya NIT- Madoto Mburahati yenye urefu wa Kilometa 1.8 na taa zake iliyogharimu sh. 8,000,000,000.
“Aidha tumefanya ukarabati kwa Barabara Mabibo Mwisho- Maungio ya Barabara ya Morogoro na taa zake yenye urefu wa kilometa 1.2 kwa gharama ya sh. 4,000,000,000,”amesema
Amesema kamati ya maendeleo ya kata iliyo chini ya usimamizi wake ilifanikisha ukarabati wa Barabara ya Ushese Kilometa 0.770, Mtaa wa Jitegemee kwa gharama ya sh. 5,000,000 ambapo ukarabati kama huo umefanyika, katika Barabara ya VINA, Mtaa wa Azimio kwa kiwango hicho hicho cha fedha.
“Pia tumefanya ukarabati wa Barabara ya Msikitini- kwa Mzee Mndenge, ukarabati umefanyika mara tatu lakini ukihusisha kipande cha Mabibo Sekondari, Zahanati ya Mabibo, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na Mwembeni Mtaa wa Mabibo Farasi. Kiasi cha shilingi milioni sitini kimetumika,”ameeleza.
Klerruu amesema ukarabati wa Kalvati eneo la AMI kwa gharama ya sh.20,000,000, ujenzi wa Kalvati eneo la Kanisa la KKKT MabiboUpogoroni kwa gharama ya sh.18,000,000 na ujenzi wa Kalvati katika eneo maarufu kwa Mzee Likonga Mabibo Farasi kwa gharama ya sh.20,000,000.
“Kubwa zaidi ni ujenzi wa kivuko cha waenda kwa miguu maarufu Kivuko cha Gonzaga kwa gharama ya ya shilingi milioni miamoja na tatu. Pia tumefanikisha ukarabati wa Barabara ya Makutano kwenda kwa Binti Kayenga, Luhanga yenye urefu wa kilometa 1.3 kwa gharama ya shilingi milioni miamoja alizotoa Rais Dk. Samia kupitia mfuko wa Jimbo,”amesema Klerruu.
Pia, Klerruu amesema chini ya Rais Dk. Samia, ujenzi wa Barabara ya Zege yenye urefu wa kilometa 1.87 kutoka TIP TOP, Makutano, Binti Kuyenga inatarajiwa kujengwa kwa gharama ya Sh. 2,500,000,000.
“Ujenzi utaanza muda wowote kuanzia sasa chini ya Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam (DMDP) Tuynamshukuru Rais Dk. Samia,”amesema.
Diwani huyo ambaye pia ni Mtaalamu wa Masuala ya Ardhi na Majenzi alieleza kufanyiwa kwa uthamini wa mali za wananchi kupisha ujenzi wa Barabara ya Mwananchi- AMI-Zahanati-Miembeni Mabibo Farasi.
“Kukamilika kwa ujenzi wa barabara hii kutaondoa msongamano wa magari kwenda Buguruni kwa wale wenye nia ya kuelekea Magomeni, Kinondoni, Oysterbay na Masaki,”ameeleza Diwani Klerruu.
Alisema kiasi cha sh.12,315,000,000 kimetumika katika sekta ya miundombinu na kwa ujumla kwa kipindi cha Mwaka 2020-2025.
Klerruu amewaomba wananchi wa Kata ya Mabibo, kuendelea kumuamini yeye, Rais Daktari Samia na CCM katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2025 kwani kazi iliyofanyika ni kubwa na Mabibo inapiga hatua kubwa kwa Maendeleo.
Uongozi wa Baraza la UVCCM Kata ya Mabibo umepokea taarifa hiyo na kumpongeza diwani huyo kwa Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuahidi ushindi mkubwa wa katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu wa Rais, Mbunge na Diwani.
Diwani Klerruu: Rais Dk. Samia ameandika historia utekelezaji miradi ya miundombinu Kata ya Mabibo
Reviewed by Gude Media
on
April 16, 2025
Rating:
