Wananchi Mwanza wahimizwa kutumia nishati ya jua
Na Mwandishi Wetu, Mwanza
Wananchi wa Mkoa wa Mwanza wamehimizwa kuanza kutumia nishati ya jua (Solar) katika juhudi za kuunga mkono kampeni ya nishati safi na salama kwa mazingira ambayo inaugwa mkono na serikali ya awamu ya sita nchini.
Rai hiyo ilitolewa na Ofisa Tarafa wa Sanyo, Wilaya ya Magu, Pepertua John kwa niaba Mkuu wa Wilaya ya Magu, Joshua Nassari wakati wa ufunguzi wa duka la Sun King katika Kijiji cha Isangijo kata Bukandwe wilayani humo ambalo ni duka lanne kwa Mkoa wa Mwanza.
Amesema kwamba ni muhimu kwa wananchi kuanza kutumia nishati safi kwa ajili ya matumizi ya umeme kwa mfano (solar) ambayo ni safi na inatunza mazingira na kuacha matumizi ya vibatari na aina nyingine ili kuendeleza kutunza mazingira.
“Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan anaendelea kuhimiza matumizi ya nishati safi na salama nchini nzima ikiwamo hii ya matumizi ya umeme jua kama njia moja wapo ya nishati safi na salama nchini nzima,” amesema.
Pepertua amesema matumizi ya vibatari yanasababisha watu kuugua macho na vifua kutokana na moshi unaotokana na vibatari hivyo wakitumia taa zinazotumia nishati ya jua ikiwemo za kampuni hiyo ya Sun King, itasaidia kuondokana na changamoto hizo.
Amesema kwamba matumizi ya nishati ya jua ni salama kwa wanafunzi kusoma pamoja na wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa uhakika nyakati za usiku.
Pepertua amesema nishati hiyo jua (solar) zinatumika pia wakati umeme umekatika na wale ambao wanaishi maeneo ambayo hayana umeme.
"Hii ni fursa kwenye maeneo ambayo bado hayajafikiwa na nishati ya umeme wa kawaida na kutumia taa hizo hususani baadhi ya vijiji wilayani humu ambavyo bado Serikali haijavifikia kwa huduma hiyo ya umeme,"amesema Pepertua.
Kwa upande wa Msimamizi wa Biashara nchini Tanzania wa Kampuni ya Sun King, Juma Mohamed, amesema kwa sasa kampuni hiyo imejikita kuuza taa zinazotumia nishati ya jua kuwasaidia wananchi kuondokana na matumizi ya nishati chafu ikiwemo vibatari vinavyotumia mafuta,hivyo wamefungua duka hilo ili kusogeza huduma kwa wananchi, kwasasa wana maduka 65 na wanatarajia zaidi ya hayo mwakani.
Mohamed amesema kampuni hiyo inaunga mkono mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kwa kuleta nishati mbadala ili kupunguza au kuzuia uzalishaji wa hewa ukaa ambayo inachangia kuharibu mazingira.
"Tupo mstari wa mbele kuhakikisha tunaunga mkono ajenda ya kidunia na Tanzania ni mdau namba moja wa kuhakikisha hewa ukaa inapungua duniani, Pia tunatekeleza ajenda ya Serikali ya kukuza uchumi wa wananchi kwa kutoa ajira kwa vijana wenye sifa ya kujua kusoma na kuandika na wenye elimu zaidi ambao wamebadilisha maisha yao kwa kiasi kikubwa", amesema.
"Tumekuwa tukitoa ajira kwa vijana ambao ni mabalozi wetu na tunaendelea kuwakumbusha kufika ofisini kwetu ili waweze kupata ajira, ambapo mpaka sasa tunao vijana kadhaa wenye shahada mbili ambao ni mabalozi wetu ambao wanafanyakazi vizuri na kujikimu kimaisha", amesema.
Kwa upande wake Balozi wa kampuni ya Sun King, Mrisho Mpoto maarufu Mjomba, amesema wananchi wamepata uelewa wa madhara ya matumizi ya nishati isiyo safi na faida ya matumizi ya nishati safi huku akisisitiza kuwa licha ya kampuni hiyo kuunga mkono suala la matumizi ya nishati safi pia imetoa ajira kwa vijana zaidi ya 3,000 nchi nzima na ni fursa zaidi kwa vijana wengine kupata ajira na kuweza kujikwamua kiuchumi.
"Lengo ni kuhamasisha watu kutoka katika matumizi ya nishati chafu hadi nishati safi,na kinara ni Rais Samia Suluhu Hassan ambaye mwenye lengo la kufikia mwaka 2034 asilimia 80 wawe wanatumia nishati safi na kufanikisha hilo ushiriki wa kampuni binafsi kama hiyo ya Sun King ni muhimu," amesema.
Naye mteja wa taa hizo za Solar kutoka Sun King Beatrice Sililo ambaye ni mkazi wa kijiji cha Wita A ameeleza namna alivyoepukana na matumizi ya nishati isiyo safi kupitia taa ya solar.
"Naitumia vizuri sana hii solar yangu ambayo inaniwezesha kuchaji simu pia nasikiliza redio maana hii taa imetengenezwa sambamba na redio, huwa ninaenda nayo katika shughuli zangu za ujasiriamali ili simu isiishiwe chaji pia usiku naitumia nyumbani", amesema.
"Ni zaidi ya miezi mitatu ninatumia hii taa za Sun King ambayo imenifanya niondokane na moshi wa kibatari na mishumaa, kwa sasa ninafurahia kuitumia maana ina mwanga wa kutosha na huwa nalipia Sh 350 tu kwa siku" amesema Sililo.
Sun King kampuni ya sola inayoongoza duniani kwa bidhaa za mfumo wa jua zinazotumika majumbani na biashara, inafuraha kutangaza uzinduzi wa maduka yao 10 mapya katika soko lake Tanzania. Tukio hili lilifanyika sambamba na uzinduzi wa bidhaa yake mpya ya HomePlus na HomePlus Pro.
Lengo kuu la Sun King ni kusambaza umeme wa jua unaobadilisha maisha na kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata bidhaa zake za kiwango cha kimataifa.
Sunking imeongeza wigo wake katika maduka 10 mapya ambayo ni Pemba, Segerea, Chalinze, Manyoni, Snawari, Kiteto, Kisesa, Rufiji, Mafinga na Soweto jijini Mbeya.
