Benki ya Standard Chartered Tanzania yaandaa kikao cha kujitolea kwa wafanyakazi kuwawezesha wajasiriamali vijana kupitia mpango wa RISE/E
Na MWANDISHI WETU
Benki ya Standard Chartered Tanzania imeandaa kikao maalum cha kujitolea kwa wafanyakazi wake kilicholenga kuwawezesha wajasiriamali vijana, kupitia mpango wake wa RISE/E, hatua inayoakisi dhamira ya Benki hiyo katika kuendeleza uchumi jumuishi kupitia ujasiriamali endelevu.
Kikao hicho kimewakutanisha wafanyakazi wa kujitolea kutoka vitengo mbalimbali vya Benki pamoja na vijana wanaonufaika na mpango wa RISE/E (Tayari kwa Ajira Jumuishi Endelevu na Ujasiriamali), ambao unatekelezwa chini ya mwavuli wa mpango wa kimataifa wa Futuremakers by Standard Chartered.
Lengo kuu la tukio mafunzo ilikuwa kutoa maarifa muhimu kwa vijana, hususan wenye biashara ndogo na za kati, waweze kukabiliana na changamoto zinazohusiana na sheria, fedha na taratibu za biashara nchini Tanzania.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Herman Kasekende, Mkurugenzi Mtendaji na Mkuu wa Idara ya Benki na Uhusiano ya Wateja wa Standard Chartered Tanzania, Herman Kasekende, amesema tukio hilo ni sehemu ya safari ya muda mrefu ya uwezeshaji.
“Hili si tukio la siku moja tu, ni hatua ya mwanzo na matumaini yetu ni kwamba mpango huu, pamoja na kikao hiki, vitawasaidia kufikiri kwa njia tofauti, kuota ndoto kubwa zaidi, kuwa na ujasiri zaidi, na kuendeleza biashara zenu zaidi”, amesema.
Mpango wa RISE/E ulizinduliwa mwaka 2024 kwa uwekezaji wa Shilingi bilioni 2.2 za Kitanzania, ukiwa na lengo la kupanua fursa za ajira kwa vijana, wakiwemo watu wenye ulemavu na kukuza biashara zinazomilikiwa na kuendeshwa na vijana.
Kupitia mpango huo, washiriki hupata mafunzo ya ujuzi wa biashara, maarifa ya kifedha na fursa ya kuunganishwa na mitandao ya kiuchumi.
Kikao cha kujitolea kimeonesha utamaduni wa ushirikishwaji ndani ya Benki, ambapo wafanyakazi walitumia maarifa yao kuwashauri wajasiriamali kuhusu mbinu bora za kuendesha biashara kwa kufuata sheria, kuwa thabiti kifedha na kujiweka tayari kwa ukuaji wa kiuchumi. Ushiriki huu unathibitisha imani ya benki katika kutumia uwezo wake wa ndani kuinua jamii.
