MAHAWANGA -TUCHANGIE CHAMA NI SEHEMU YA KUJENGA UMOJA, UMILIKI NA USHINDI UTOKANAO NA WANACHAMA
Mjumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa UWT Mkoa wa Dar es Salaam, Janeth Mahawanga amekipongeza Chama Cha Mapinfuzi (CCM), kinachoongozwa na Mwenyekiti Dk. Samia Suluhu Hassan na Katibu Mkuu Dk. Emmanuel Nchimbi kwa wazo jema bora la kuchangia kampeni za Chama ni uwekezaji katika mustakabali wa Taifa.
Akizungumza na Uhuru digital, alisema kila mpango, mkubwa au mdogo ni ishara ya mshikamano, mashirikiano na imani kwa dira na sera wanazozitetea.
"Hii ni nafasi yetu sisi wanachama, marafiki na wapenzi wa CCM kuhakikisha chama chetu kinaendelea kushinda na kutekeleza mipango ya maendeleo kwa manufaa ya watanzania wote ndani ya Taifa hili, kwani ilani inayoenda kutekelezwa haina mipaka katika kuboresha na kuchochea maendeleo ya wananchi wote bila kujali itikadi zetu, dini wala makabila yetu," alisema.
Alisema kila mwanachama na mwananchi anaposhiriki kuchangia kampeni hizo anaonyesha moja kwa moja kuwa anaimani na dira, sera sambamba na wagombea wa Chama kujenga hari na mshikamano miongoni mwa wanachama, wapenzi na wafuasi wa Chama.
Alieleza kuwa, kuchangia kunawezesha wananchi kuwa sehemu ya ushindi na inasaidia kujenga umiliki wa chama kwa kuonyesha kwamba chama ni mali yao na ushindi wake ni ushindi wao.
Aliwasihi wanachama wote, wapenzi na marafiki wote wa CCM kuendelea kuchangia chochote walichonacho bila kujali ukubwa au udogo, itakuwa ni sehemu ya msingi wa ushindi, umoja, mshikamano na maendeleo tunayoazimia.
