Wasimamizi wasaidizi ngazi ya kata watakiwa kuendeleza utendaji kazi kwa uadilifu, uaminifu na uzalendo
Na MWANDISHI WETU
MSIMAMIZI wa Uchaguzi Jimbo la Igunga na Manonga wilayani Igunga mkoani Tabora, Hamisi Hamisi amewaasa Wasimamizi Wasaidizi ngazi ya kata kuendeleza utendaji wao wa kiuadilifu, uaminifu, uzalendo, uchapakazi na uaminifu.
Hamisi ametoa rai hiyo wakati wa mafunzo kwa Wasimamizi hao yaliyofanyika katika ukumbi wa Maxweli mjini Igunga.
“Nyinyi mliopo hapa mmeteuliwa kwa mujibu wa sheria, hivyo mnaowajibu wa kikatiba na sheria kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani katika maeneo yenu’’ amesisitiza.
Aidha, amewakumbusha wamebeba dhamana kubwa, nyeti na muhimu kwa mustakabali wa Tanzania Bara, hivyo wanategemewa kuzingatia utendaji wao na kuwajibika ipasavyo kipindi chote cha utumishi wao katika Tume Huru ya Uchaguzi (INEC).
