BARRICK BULYANHHULU YAWEZESHA MAFUNZO YA KANUNI ZA WAJIBU WAMILIKI WA LESENI ZA MADINI KWA JAMII VIONGOZI WA WILAYA YA MSALALA NA NYANG'HWALE






Na Mwandishi Wetu 


Katika kuboresha utekelezaji wa Miradi itokanayo na uwajibikaji wa jamii (CSR) Mgodi wa Barick Bulyanhulu kwa kushirikiana na Tume ya Madini  wameendesha mafunzo kwa watumishi wa  Halmashauri wilaya za  Nyang’hwale  kutoka mkoani Geita na Msalala  mkoani  Shinyanga juu ya Kanuni za wajibu wa wamiliki wa leseni za madini kwa jamii CSR za mwaka 2023.


Mafunzo hayo ya siku mbili yaliyofanyika  katika Mgodi wa Bulyanhulu,  mwishoni mwa wiki yalifungwa na Mkuu wa  wilaya ya Nyang’hwale, Grace Kingalame, ambaye aliupongeza mgodi huo kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo yatawasaidia waatalamu kutoka halmashauri ya wilaya hizo 2  kutekeleza kwa ufanisi Miradi ya Kijamii inayotekelezwa kwa fedha kutoka Barrick Bulyanhulu.


 “Tunaipongeza Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kuwezesha upatikanaji wa kanuni hizi, na nina imani kupitia mafunzo haya miradi yote itasimamiwa vizuri zaidi katika kipindi cha mwaka ujao ili kufanikisha lengo lililokusudiwa na kunufaisha wananchi.


Naye Mkurugenzi  wa Halmashauri ya Msalala, Khamis Katimba, ameishukuru Barrick  Bulyanhulu kwa kuandaa mafunzo hayo  ambapo amesema Halmashauri yake inanufaika kwa kiasi kikubwa na uwekezaji uliofanywa na Mgodi huo  kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo imetekelezwa katika halmashauri hiyo.


Katimba,  amesema  ni muhimu  miradi ya CSR kuzingatia kubadilisha maisha ya wananchi walio maeneo yaliyo na uchimbaji wa madini na kuhimiza  uaminifu na uadilifu kwa maofisa wanaosimamia miradi hiyo  ili kuleta tija kwa wananchi huku akiainisha changamoto ambazo zilikuwa zinatokana na kutokuwa na kanuni kama vile miradi kutotekelezwa kwa wakati, kupishana kwa mtazamo kati ya halmashauri na migodi pamoja na uelewa mdogo wa masuala ya CSR.

 

Akiwasilisha kanuni hizo  Mhandisi Migodi kutoka Tume ya Madini Makao Makuu Mackenzie Mabula, alisema kuwa  kanuni hizo mpya zitatumika kwa wamiliki wa leseni za madini ambapo zinatarajiwa kuwasaidia sana waatalamu na wasimamizi wa miradi ambayo itatekelezwa kupitia CSR.

Aidha amezitaka Halmashauri hizo kuzifuata kanuni hizo ili kurahisisha uandaaji na utekelezaji wa Miradi.


“Niwaombe sana kanuni hizi ni rafiki sana katika utekelezaji wetu hivyo tuzifuate inavyotakiwa kwani awali tulikuwa na sheria pekee jambo ambalo lilikuwa linawapa ugumu kuzichambua sheria zote sasa tutumie kanuni hizi kutekeleza Miradi yetu", amesema Mabula.


Kwa Upande wake Meneja wa wa Mazingira na Uhusiano ya Mgodi wa Barrick Bulyanhulu,  Agapiti Paul,  ameziomba Halmashauri hizo kuendelea kushirikiana na mgodi ili kufanikiwa kukamilisha miradi kwa wakati  ili wananchi waweze kunufaika na uwekezaji uliofanywa na Mgodi huo.

Wataalamu kutoka Halmashauri za wilaya  za Msalala na Nyang’hwale wakifuatilia mada wakati wa mafunzo ya kanuni  mpya za wajibu wa wamiliki wa leseni za madini kwa jamii  za mwaka 2023 (CSR), yaliyoandaliwa na Mgodi wa Barrick Bulyanhulu kwa kushirikiana na Tume ya Madini yaliyofanyika mgodini hapo mwishoni mwa wiki.



Meneja wa  Mazingira na Uhusiano ya Jamii wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu,  Agapiti Paul, akichangia mada wakati wa mafunzo ya kanuni  mpya za wajibu wa wamiliki wa leseni za madini kwa jamii  za mwaka 2023 (CSR) yaliyoandaliwa na Mgodi wa Barrick Bulyanhulu kwa kushirikiana na Tume ya Madini yaliyofanyika mgodini hapo mwishoni mwa wiki.


Mkurugenzi  wa Halmashauri ya Msalala, Khamis Katimba akichangia mada wakati wa mafunzo ya kanuni  mpya za wajibu wa wamiliki wa leseni za madini kwa jamii  za mwaka 2023 (CSR) yaliyoandaliwa na Mgodi wa Barrick Bulyanhulu kwa kushirikiana na Tume ya Madini yaliyofanyika mgodini hapo mwishoni mwa wiki.