Mbeto: Rais Dk. Samia amethibitisha uzalendo na uungwana alionao
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Chama Cha Mapinduzi kimesema hotuba iliotolewa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan alipozungumza na Wazee wa Mkoa wa Dar Es Salaam ,ameonyesha kina cha uelewa alionao, ukomavu na uungwana wake kisiasa .
Pia CCM kimeitaja hotuba hiyo imeshiba uzalendo, historia na yenye kuhimiza haja na nia ya kuendeleza dhima ya Umoja wa Kitaifa .
Hayo yameelezwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar , Idara ya Itikadi , Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis aliyeitaja hotuba hiyo kuwa imeweka msimamo thabit wa kulinda uhuru , Amani na utulivu.
Mbeto alisema matamshi ya Rais Dk Samia yamewataka viongozi wa madhehebu za Dini kuacha kuingilia medani za Siasa na kuipangia hatma Serikali na kusisitiza kuwa Tanzania haina Dini bali wananachi wake ndio wenye imani za Dini.
Alisema hotuba hiyo ya Rais licha ya kuwa ni ya kizalendo ,imetoboa ukweli unaowataka Watanzania wote kujiona wako sawa mbele ya katiba na kuwataka waendelee kushi bila chuki,hasama au ubaguzi .
"Rais Dk Samia ametoa hotuba inayohimiza shime ya Umoja, Uzalendo na upendo kwa Taifa. Amewataka viongozi wa Dini waendelee kuwalea kiroho waumini wao bila ishara ya kulivuruga Taifa " Alisema Mbeto
Aidha, Mwenezi huyo alisema Rais alihimiza ipo haja ýa watu kutotofautiana kwani njia pekee kupata muafaka ni kukaa pamoja mezani, kujadiliana , kuzumgumza hatimae kupata suluhisho .
'Kila jambo gumu katika chini ya jua yoyote linazungumzika mezani . Rais Dk Samia hilo ameliweka bayana na kusisitiza hata marekebisho ya katiba mpya ýanawezekana na kufikia tamati "Alieleza
Pia Katibu huyo Mwenezi aliitaja nia ya Serikali ya CCM si kupendelea upande wowote wa madhehebu za dini au vyama vya kisiasa ,badala yake aliwataka watanzania wote kuheshimu sheria za nchi .
Mbeto alisema ana hakika hotuba ya Rais Samia imefungua ukurasa mpya ambao utawaweka watanzamia wote mahali pamoja kama ilivyo utamaduni , mila na desturi ya Watanzania .
'Rais Dk Samia ameonyesha ushupavu na ujasiri akiwa ndiye mkuu wa Nchi. Pia ametumia muda wake kuyaeleza mataifa rafiki mipaka yao wakiwa washika dau wa maendeleo bila kuingilia uhuru wa Taifa letu, alisema Mbeto
Reviewed by Gude Media
on
December 02, 2025
Rating:
