DIWANI KIGAMBONI AWATAKA VIJANA KUMUENZI BABA WA TAIFA KWA VITENDO

 



Na Mwandishi Wetu


WANANCHI wa Kata ya Kigamboni, wamekumbushwa kumsoma na kumjua Rais wa Kwanza wa Tanzania, Hayati Julius Nyerere, kutokana mchango wake mkubwa wakati wa uongozi.


Hayo yalisemwa na Diwani wa kata hiyo, Dotto Msawa, baada ya kumaliza kufanya usafi na mazoezi wakati wa kumbukizi ya Baba wa Taifa Julius Nyerere, wilayani Kigamboni, Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki.


Msawa alisema vijana lazima wamjue muasisi wa taifa la Tanzania, ndiyo maana wameamua kutumia siku hiyo kufanya usafi na kuwakumbusha vijana alikuwepo kiongozi mwenye maono makubwa na mzelendo wa kwanza hapa nchini.


"Lengo la kufanya usafi na mazoezi ni kuwakusanya vijana pamoja na kuwakumbusha kazi alizokuwa akifanya Hayati Baba ya Taifa, pia vijana wamsome kumfahamu kwani alikuwa kiongozi bora wa kuigwa nchini na bara la Afrika.


Pia Msawa, ameomba Viongozi na Watanzania wote kumuunga mkono Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ya kuleta maendeleo kwa wananchi.


Alisema katika uongozi wa Rais Samia, Kata ya Kigamboni, imepokea fedha nyingi za utekelezaji wa miradi mbalimabli ya maendeleo zikiwemo sekta za afya, elimu na barabara.


"Kata ya Kigamboni tunamshumuru rais wetu, tumepata fedha nyingi za ujenzi wa shule, barabara za mitaani kwa kiwango cha lami na sekta afya, hiyo inaonyesha namna anavyotupenda wananchi wake wa Kata ya Kigamboni, tunamshukuru sana rais wetu, pia Kata ya Kigamboni tunampongeza kwa kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa nchini India hivi karibuni", alisema.


Kwa upande wa Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kigamboni, Mariam Muya, alisema wanamkumbuka Baba wa Taifa kwa kufanya usafi nakushiriki mazoezi ikiwa ni kuwakumbusha vijana kumfahamu Hayati Julius Nyerere, pia vijana wanaweza kujifunza mambo mazuri ya kiungozi kupitia kwake.


Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Feri, Juma Mwingamno, alisema kumbukizi ya Baba wa Taifa ni kuwahamasisha vijana wasiomjua muasisi wa taifa, wamtambue kutokana kazi za uongozi wake.


"Lengo letu la kufanya usafi na mazoezi ni kuwahamasisha vijana wetu kumtambua mtangulizi kiongozi wa taifa hili Baba wa Taifa, Julius Nyerere, tumeweza kufanya usafi maeneo yote ya mtaa wangu, pia tumeshiriki kufanya mazoezi ya kujenga afya zetu", alisema.