JOKATE ATEULIWA KUWA KATIBU MKUU UWT



Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), iliyokutana katika kikao maalumu, Oktoba Mosi, Dar es Salaam, imefanya uteuzi kwa Makatibu wakuu wa Jumuiya za Umoja wa Wanawake (UWT) na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).


Taarifa kwa umma iliyotolewa na Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Sophia Mjema,   imeeleza katika kikao hicho, Kamati Kuu imemteua Jokate Mwegelo, kuwa katibu Mkuu wa UWT, kabla uteuzi huo, Jakate alikuwa mkuu wa Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga.


Pia Kamati Kuu imemteua Fakii Lulandala kuwa katibu mkuu wa UVCCM, kabla uteuzi huo Lulandala alikuwa Mkuu wa Wilaya Momba, mkoani Songwe.


Katika hatua nyingine, Kamati Kuu imemteua Hamad Khamis Hamad, kuwa Mgombea wa CCM wa nafasi ya Uwakilishi Jimbo la Matimbwe.


Vile vile Kamati Kuu imewashukuru na kuwapongeza wanachama wote wa CCM na wananchi wote wa Jimbo la Mbalali kwa kumchagua Bahati Ndingo, kuwa Mbunge wao katika uchaguzi mdogo uliyofanyika Septemba 20.


Pia Kamati Kuu imempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kutokana na ziara aliyoifanya katika Mikoa ya Lindi na Mtwara, ambayo ilikuwa na mafanikio makubwa sana. Katika ziara hiyo na mambo mengine Rais alikagua utekelezaji wa Ilani ya 2020/2025, kusikiliza na kuzitafutia ufumbuzi changamoto za wananchi.


Kamati Kuu imempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa namna anavyoiongoza katika kutekeleza Ilani ya CCM.