MRADI WA USANIFU BWAWA LA FARKWA WASAINIWA, KUJAZA MAJI LITA MILIONI 440 WILAYANI CHEMBA


Waziri wa Maji, Jumaa Aweso




Na Mwandishi Wetu

Wizara ya Maji imeingia mkataba wa mwaka mmoja na  Kampuni ya SU-YAPI Engineering Consulting Inc. kufanya kazi ya usanifu wa ujenzi wa Bwawa la Farkwa,  litakalojengwa wilayani Chemba, ambalo litanufaisha wakazi wa wilaya za Chemba, Chamwino, Bahi na Jiji la Dodoma.


Mkataba umesainiwa Oktoba 23, 2023 ikiwa ni awamu ya kwanza, mradi ambao utagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 312, kwa ujenzi wa Bwawa lenye ujazo wa lita za maji milioni  440.


Waziri wa Maji  Mhe. Jumaa  Aweso (Mb), ameshuhudia hafla hiyo na amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha shilingi bilioni 312, ili kuondosha tatizo la maji katika  Wilaya nne za Mkoa wa Dodoma, wakazi wake wapate majisafi, salama na yenye kutosheleza.


Mhe. Aweso amewahakikishia wananchi wa Wilaya ya Chemba, Wizara ya Maji itatekeleza mradi huo kwa kuwashirikisha wananchi wawe sehemu ya mradi na ujenzi ukamilike kwa wakati kama ilivyopangwa na Serikali.


Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira,  Mhe. Jackson Kiswaga,  Mbunge wa Jimbo la Kalenga, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia kwa kujitoa na kupeleka fedha shilingi Bilioni 312 za ujenzi wa  awamu ya kwanza ya bwawa hilo.


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amewaomba wananchi wa Wilaya ya hiyo wawe na imani na serikali yao na kwamba tatizo la upatikanaji wa maji litakwisha, kwani Serikali imedhamiria kumaliza kabisa changamoto ya uhaba wa maji kwa wakazi wa Wilaya ya Chemba.