MUHIMBILI (UPANGA & MLOGANZILA) KUANZISHA HUDUMA YA 3D PRINTING KWA WAGONJWA WA KINYWA NA MENO

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi






Hospitali ya Taifa Muhimbili (Upanga na Mloganzila) kwa kushirikiana na Taasisi ya Miracle Corner World (MCW) kutoka nchini Marekeni inatarajia kuanzisha huduma ya matibabu ya magonjwa ya kinywa na meno kwa kutumia teknolojia ya 3D printing ambayo inarahisisha utengenezaji wa meno bandia, vifuniko vya meno (Crown) na utengenezaji wa Taya zilizoathirika na ajali na magonjwa mbalimbali.


Utengenezaji wa meno, vifuniko vya meno na Taya kwa kutumia Teknolojia ya 3D Printing unatumia muda wa dakika 8 hadi kumi, tofauti na sasa ambapo ili mtu atengenezewe jino au taya inachukua muda wa wiki mbili huku ikihusisha michakato mbalimbali mbalimbali ya kimaabara.


Hayo yalibainishwa  na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi alipokutana na uongozi wa Taasisi ya MCW kwa lengo la kujadili namna ya kuhakikisha huduma hiyo inaanzishwa haraka katika Hospitali ya Upanga na Mloganzila.


Prof. Janabi aliangiza Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji Dkt. Rachel Mhavile na timu ya wataalamu mbalimbali kuhakikisha  mchakato wa ushirikiano huo unaharakishwa ili kufanya huduma hizi zianze kutolewa na wananchi wanufaike.


Alisema huduma hizi zikianza zitafanya Muhimbili (Upanga & Mloganzila ) kuwa hospitali ya kwanza ya Umma nchini kutoa huduma hiyo ya kisasa .


“Kupitia ushirikianao huu wataalamu wetu watajengewa uwezo jambo ambalo litaendelea kuboresha huduma ya afya ya kinywa na meno na kurahisisha huduma ya utengenezaji wa meno bandia kwa watu wanaohitaji huduma hiyo” alieleza Prof. Janabi 


Kwa Upande wake mmoja wa viongozi wa Taasisi ya Miracle Corner Bi Marion Bergman ameahidi kutoa ushirikiano kwa kuwajengea uwezo wataalamu wa Muhimbili ili waweze kutoa huduma hiyo kwa ufanisi zaidi.