Na Mwandishi Wetu
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Juma Simba 'Gadafi', amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji Dar es Salaam, Jomaary Satura, kuwachukulia hatua wakandarasi wasiokuwa na uwezo wa kutekeleza miradi ujenzi kwa wakati.
Gadafi ametoa wito huo, wakati Kamati ya Siasa Mkoa wa Dar es Salaama, ilipokagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Amesema Mkurugenzi akae na wakandarasi hao wapitie mikataba yao ambao uwezo wao wa kufanya kazi ni mdogo waondolewe haraka, kwani haiwezekani fedha za Watanzania zitumike vibaya, Chama hakitakubali kuona miradi haikamiliki kwa wakati.
Gadafi amesema wakandarasi wasiokuwa na uwezo wa kutekeleza muradi ni maadui wa wananchi, pia maadui wa Chama Cha Mapinduzi pamoja na kuwachonganisha na serikali yao.
"Wakandarasi hawa ni maadui wa wananchi na maadui wa Chama, hivyo wachukuliwe hatua za kisheria, kusiwe shamba la bibi kwa mkandarasi ambao hawana uwezo wa kukamilisha miradi ya maendeleo naomba Mkurugenzi wachukulie hatua za kisheria, amesema.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Jiji, Jomaary Satura, amesema baadhi ya wakandarasi wazawa hawana uwezo wa kutekeleza miradi kwasababu wanatumia fedha za utekelezaji miradi kujinufaisha binafsi.
Amesema fedha zipo lakini tatizo ni wakandarasi wenyewe na hatuta wavumilia tena kwa mkandarasi ambaye uwezo wake mdogo wa kumaliza miradi kwa wakati.
"Wajiandae wakandarasi wabovu na hatutawalea tena, sasa tutaenda katika taratibu za mikataba yao, kwani wakipewa fedha za awali za kutekeleza mradi wanaenda kutumia katika miradi mingine au wanatumia katika vitu vyao binafsi, sasa imetosha wajiandae kuondoka", amesema.
Kamati hiyo imekagua miradi mbalimbali ikiwemo, mradi ujenzi wa Shule ya Sekondari Bonyokwa, Shule ya Sekondari Kipunguni, ujenzi wa barabara ya lami Pugu Majoe na ujenzi wa jengo la Wazazi katika Hospitali ya Kivule.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Juma Simba 'Gadafi', akipokea taarifa kutoka kwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Bonyokwa, baada ya kukagua ujenzi wa shule hiyo. |
Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaa, Jomaary Satura, akimuonyesha MNEC Juma Simba 'Gadafi', majengo ya Hospitali ya Kivule, wakati kamati hiyo ikikagua miundombinu ya hospitali hiyo. |