VYUO VIPYA VYA WATU WENYE ULEMAVU KUJENGWA RUVUMA, KIGOMA NA SONGWE - WAZIRI MKU




Aiagiza Wizara ya Uchukuzi iweke taa za barabarani kwenye makutano ya reli na barabara

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeanza ujenzi wa vyuo vipya vitatu vya ufundi stadi na marekebisho kwa watu wenye ulemavu katika mikoa ya Ruvuma, Kigoma na Songwe ili kusogeza huduma hii karibu na wananchi.


“Mradi huu katika mwaka wa fedha 2022/2023 ulitengewa shilingi bilioni tatu na katika mwaka 2023/2024 umetengewa shilingi bilioni tatu nyingine. Tayari miundombinu ya madarasa, mabweni, nyumba za watumishi na ofisi za walimu zimeanza kujengwa sambamba na karakana ambazo hazihitaji majengo maalum,” amesema.


Ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Desemba 2, 2023) wakati akizungumza na washiriki na wadau mbalimbali kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani katika ukumbi wa Halmashauri ya Dodoma Jiji uliopo Mji wa Serikali, Mtumba, Dodoma.


Waziri Mkuu ambaye alikuwa akielezea jitihada za Serikali za kuimarisha ustawi wa jamii ya watu wenye ulemavu nchini, amesema Serikali imetoa shilingi milioni 960 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni tisa kwenye shule nane zenye wanafunzi wenye mahitaji maalum katika mikoa ya Shinyanga (Shule ya Buhangija); Njombe (Shule ya Idofi) na Arusha (Shule ya Longido). Mikoa mingine ni Lindi (Shule ya Mtanga); Tabora (Shule ya Goweko); Singida (Shule ya Darajani); Manyara (Shule ya Songambele) na Rukwa (Shule ya Msanzi).


“Kama mtakumbuka, fedha hizo zilitengwa kwa ajili ya sherehe za miaka 61 ya Uhuru mnamo Desemba, 2022 lakini Mheshimiwa Rais wetu kwa mapenzi makubwa alielekeza zikajenge miundombinu ya shule hizo.”


Akifafanua kuhusu kuimarisha upatikanaji wa miundombinu ya elimu, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kumalizia ujenzi wa shule maalum ya Mbuye iliyoko Chato, mkoani Geita yenye “blocks” tatu ikiwemo awali, msingi na sekondari ya chini na juu ambayo imekamilika kwa asilimia 95 na ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,200.


Kuhusu maboresho ya utoaji wa huduma za afya, Waziri Mkuu amesema katika kipindi cha mwaka 2022/2023, Serikali imetoa huduma za afya kwa makundi maalumu kwa msamaha katika vituo vya kutolea ambapo jumla ya wahitaji 5,225,761 walipatiwa huduma kwa msamaha wakiwemo watu wenye ulemavu, na huduma hizo zimegharimu sh. bilioni 570.67.


Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Uchukuzi ihakikishe kuwa kila palipo na makutano ya reli na barabara pawekwe taa za kuashiria au kifungio cha automatiki cha kuzuia na kuruhusu magari ili kunusuru maisha ya Watanzania.


“Kutokana na kuwepo matukio ya ajali za mara kwa mara zinazohusisha treni na vyombo vingine vya moto, TARURA na TANROADS washirikiane na Shirika la Reli nchini kuhakikisha maeneo yote yenye makutano yanaimarishwa kwa kuwekwa mifumo au alama zenye tahadhari ya kutosha kuweza kudhibiti matukio ya namna hiyo. Aidha, wamiliki wa vyombo pamoja na madereva wote wazingatie alama za barabarani kwa ukamilifu,” amesisitiza.