WAZIRI MKUU AZINDUA RIPOTI YA UTAFITI VIASHIRIA VYA UKIMWI

 



Yabainisha maambukizi mapya kwa watu wazima yanazidi kupungua

Kiwango cha kufubaza VVU kimeendelea kukua na kufikia asilimia 78


 


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua ripoti ya utafiti wa viashiria vya UKIMWI ambayo inaonesha maambukizi mapya miongoni mwa watu wazima wenye umri zaidi ya miaka 15 yanaendelea kupungua.


“Maambukizi mapya miongoni mwa watu wazima wenye zaidi ya miaka 15 yanaendelea kupungua kutoka watu 72,000 waliokuwepo mwaka 2016/2017 hadi watu 60,000 kwa mwaka 2022/2023. Hii ni sawa upungufu wa asilimia 0.18 ambapo asilimia 0.24 ni wanawake na asilimia 0.11 ni wanaume,” amesema. 


Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Desemba mosi, 2023) wakati akizungumza na mamia ya wananchi waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika kwenye viwanja vya shule ya sekondari ya Morogoro, mjini Morogoro.


Amesema Serikali iliamua kufanya utafiti kwa lengo la kujua hali ya sasa ya VVU na UKIMWI ilivyo hapa nchini na matokeo yameonesha kuwa Tanzania imepata mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya UKIMWI.


Utafiti huo unaotambulika kama Utafiti wa Viashiria vya UKIMWI kwa mwaka 2022/2023 unapima matokeo ya mwitikio wa kitaifa wa UKIMWI nchini miongoni mwa watu wazima wenye umri wa kuanzia miaka 15 ukiwa na lengo la kukadiria kiwango cha maambukizi mapya ya VVU, ushamiri wa VVU, ufubazaji wa VVU kwa watu wanaoishi na VVU na utumiaji wa dawa kitaifa na kimikoa. 


“Utafiti umebaini kuwa kiwango cha kufubaza VVU kimeendelea kukua ambapo kwa sasa ni wastani wa asilimia 78 ambapo kwa upande wa wanawake kiwango kimekua kwa asilimia 80.9 na wanaume asilimia 72.2 ikilinganishwa na asilimia 52 iliyokuwepo kulingana na utafiti wa mwaka 2016/2017.”


“Kiashiria hiki ni muhimu kwa sababu mtu anapokuwa amefubaza VVU anakuwa na afya njema na hatasumbuliwa na UKIMWI pamoja na magonjwa nyemelezi. Pia anapofikia kiwango ambacho virusi havionekani maabara, basi hataweza kuambukiza VVU kwa wengine,” amesema.


Kuhusu kiwango cha ushamiri wa VVU kwa umri kuanzia miaka 15 na zaidi kwa mikoa ya Tanzania bara, Waziri Mkuu amesema utafiti umeonesha kuwa, kinaanzia asilimia 1.7 kwa mkoa wa Kigoma hadi kufikia asilimia 12.7 kwa mikoa ya Njombe, Mbeya na Iringa. “Mkoa wa Njombe una viwango vya ushamiri zaidi ya asilimia 9 sawa na mara mbili ya kiwango cha Taifa. Kwa upande wa Zanzibar, yanaonesha unaanzia asilimia 0.2 katika Mkoa wa Kaskazini Pemba hadi asilimia 0.8 Mkoa wa Kusini Unguja,” amesema.


Akitoa maagizo mahsusi, Waziri Mkuu amewataka vijana wajitambue na kuthamini maisha yao kwa kujikinga na maambukizi mapya ya VVU. “Wadau wote wekeni kipaumbele katika kundi hili muhimu ili kulinusuru na athari za UKIMWI.”


Pia amewataka watu wanaoishi na VVU waendelee kutumia dawa za ARV kwa ufuasi sahihi bila kuacha ili kufubaza VVU na kuimarisha afya zao. “Taifa linawategemea, Serikali itaendelea kuhakikisha huduma za ARV nchini zinapatikana.”


Ameitaka mikoa na wilaya zote nchini itekeleze maelekezo ya kufanya Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani na kutoa huduma stahiki kwa wananchi. “Kila mkoa uandae taarifa ya maadhimisho itakayoainisha huduma mbalimbali za kijamii na kuiwasilisha kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI,” amesisitiza.


Ametumia fursa hiyo kuwaomba viongozi wa dini, wa siasa na wa kimila watumie majukwaa waliyonayo kuendelea kusema na kukemea taarifa za ubaguzi dhidi ya WAVIU na kuhimiza upendo na huruma kwao.

 

Mapema, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama alisema ofisi yake kwa kushirikiana na ofisi ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) pamoja na Waziri wa Afya watajipanga kuhakikisha wanawalinda vijana wa Tanzania dhidi ya janga la UKIMWI.


Naye, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema ili kukabiliana na kasi ya kuenea kwa maambukizi wa VVU, wizara yake imezindua mpango wa kuoanisha VVU, magonjwa ya ngono na homa ya ini kwani kuna ushabihiano mkubwa wa njia za maambukizi za magonjwa hayo.


Amesema hatua hiyo imekuja baada ya kubaini kuwa asilimia 4.4 ya Watanzania wana maambukizi ya magonjwa ya ini.


Akielezea mpango wa wizara kufikisha huduma ya afya kwa ngazi ya jamii, alisema wizara hiyo inatarajia kuajiri wahudumu wa afya ya jamii 137,000 ambao watafanya kazi kuanzia ngazi ya mitaa na vitongoji.