Na John Jayros
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, John Mongella amesema Tamasha la kumuenzi Bibi Titi Mohamed, pia linatumika kuenzi kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Mongella ameyasema haya Desemba 13, 2024 wakati akifungua rasmi tamasha la mwaka huu la Bibi Titi, IKwiriri wilayani Rufiji, huku akimpongeza Mbunge wa Jimbo hilo, Mohamed Mchengerwa kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya ya kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo hilo.
“Ndugu wananchi wa jimbo la Rufiji, sisi kama Chama tunaliona jimbo hili ni miongoni mwa majimbo salama ambayo yamefanya kazi nzuri kwa wananchi wake, hivyo mtambue mna mbunge bora”, amesema.
Pia Mongella ametoa rai kwa viongozi wa CCM kote nchini kuendelea kushughulikia kero za wananchi na kuachana na kufikiria ushindi uliopita wa CCM badala yake kuendelea kuwaletea mandeleo.
Kwa upande wake, Mchengerwa amemshukuru na kumpongeza Rais Dk. Samia kwa kazi kubwa ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Wilaya ya Rufiji na maono makubwa na mapinduzi aliyoyafanya katika kipindi kifupi cha uongozi wake.
“Naomba kuchukua nafasi hii kumshukuru Rais kwa upendo wake kwa kuifanya Wilaya ya Rufiji kuwa Mamlaka ya Mji Mdogo hivyo kusaidia kunufaika na fedha za Benki ya Dunia” amesema Mchengerwa.
Katika ufunguzi huo, Halimashauri ya Wilaya ya Rufiji, imetiliana saini mkataba wa ujenzi wa jengo la ofisi ya kisasa ya Wilaya hiyo lenye gharama ya zaidi ya Bilioni kumi.
Aidha, Mchengerwa ametumia jukwaa hilo kuwahakikishia wananchi wa Rufiji kuendelea kutambua mchango wa hayati Bibi Titi na viongozi waliotangulia na kwamba atashirikiana nao katika kuwaletea maendeleo ya kweli.
Amewashukuru Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) kwa kuendelea kutambua mchango wa Bibi Titi na kuahidi kuendelea kuadhimisha kila mwaka.
Tamasha la nne la Bibi Titi Mohamed la mwaka huu, limeadhimishwa kwa kuelezea kazi kubwa inayofanywa na serikali, ambapo kesho linafikia kilele chake.