RAIS DK.MWINYI AZINDUA BODI MPYA YA BENJAMİN MKAPA FOUNDATION



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameishauri Bodi mpya ya Wadhamini ya Taasisi ya Benjamin William Mkapa kuhakikisha inaendelea kuwa chombo cha kuaminika na Watanzania kwenye kuimarisha sekta ya afya ndani na nje ya nchi kama ilivyo Dira ya Taasisi hiyo.

Rais Dk Mwinyi ameyasema hayo leo, alipozindua Bodi Mpya ya Benjamin Mkapa Foundation ( BMF) katika hafla iliofanyika Ukumbi wa BMF Kawe, jijini Dar es Salaam.

Rais Dk. Mwinyi ambae ni Msarifu wa taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation, ameeleza kuwa ni vema kwa sifa za wajumbe wa taasisi hiyo, kuendelea kudumu ndani ya taasisi kuwavutia washirika zaidi na kuhakikisha ukuaji endelevu wa kuwahudumia walengwa wa taasisi hiyo.

Pia, Rais Dk. Mwinyi alifafanua kuwa, Mpango Mkakati wa Taasisi hiyo utakaodumu kuanzia Julai 2024 hadi Juni 2030 utategemea Bodi na Menejimenti katika kutekeleza na kufikia malengo yaliowekwa na kusisitiza umuhimu wa kudumisha rekodi nzuri ya utawala Bora, Uongozi mahiri, Utendaji wa kazi wa taasisi hiyo.

Akizungumza katika Hafla hiyo, Mwenyekiti Mpya wa BMF Balozi Liberata Mulamula ameahidi kwa bodi hiyo kufanya kazi kwa karibu na Serikali zote mbili za SMT na SMZ katika kufikia malengo na Dira ya taasisi hiyo.