Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. John Jingu ameipongeza Hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana na jinsi ilivyojipanga kila siku kutoa huduma za dharura zinazopokelewa kutoka Hospitali mbalimbali nchini, watu binafsi na wale wanaoletwa na Jeshi la Polisi na kupata huduma kupitia Idara ya Tiba na Magonjwa ya Dharura pamoja na Kitengo cha Dharura kwa Kina Mama Wajawazito.
Hayo ameyasema leo alipofanya ziara Hospitalini hapo kuangalia hali ya utoaji huduma hususani mfumo mzima wa utoaji huduma za tiba kwa wagonjwa wanaopata dharura mbalimbali ikiwemo ajali au kuumwa ghafla na kuongeza kuwa hospitali imejipanga vizuri na imeanza kuchukua hatua kutokana na kuwa na mfumo unaoonesha taarifa zinavyokuja kutoka kwa wananchi, kufanyiwa kazi na wananchi kuhudumiwa na kuahidi kuimarisha zaidi eneo hilo.
“Nawapongeza wenzetu Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kazi kubwa mnayoifanya katika kuhudumia wananchi, nasi tupo hapa kwenye mradi wa kuimarisha huduma za matibabu ya dharura ambalo ni eneo muhimu kwa sababu ndiyo hasa linasaidia kuokoa maisha inapotokea dharura ambayo inaweza kuwa ajali au ugonjwa wa ghalfa au jambo lolote lile la kiafya” amesisitiza Dkt. Jingu.
Ameeleza kuwa Serikali ilisambaza vifaa na magari mengi ya utoaji huduma za dharura kwa hospitali mbalimbali nchini na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliielekeza Wizara kuhakikisha magari yote na vifaa vilivyosambazwa vinafanya kazi iliyokusudiwa na magari yaratibiwe kwa karibu zaidi.
*Katika ziara hiyo ya kufuatilia utekeleza wa maagizo ya Mhe. Rais, Dkt. Jingu amesema kuwa ili hayo yafanyike vizuri, inabidi kuimarisha mifumo ya mawasiliano ya kidigitali ya kufuatilia magari pamoja na vifaa vingine ili kuweza kuratibu huduma ya magari ya wagonjwa ipasavyo na kuhakikisha vinafanya kazi wakati wote na ipasavyo.
Aidha aliongeza kuwa huduma za dharura hazitaishia tu kwenye magari bali pia mfumo huo uwezeshe watoa huduma wa dharura au anayepatiwa huduma kutoa taarifa za msingi za mgonjwa ili mgonjwa huyo anapofika hospitali apate huduma haraka kutokana na taarifa zake kuwafikia mapema watoa huduma katika hospitali na kuwawezesha kuwa tayari kumhudumia mara tu anapopokelewa* .
Idara ya Tiba na Magonjwa ya Dharura inahudumia wagonjwa 150 hadi 200 ambapo kati yao 100 ni rufaa za simu kutoka hospitali mbalimbali, mtu mmoja mmoja na rufaa binafsi kutoka nyumbani ambapo kwa upande wa Kitengo cha Dharura kwa Kina Mama Wajawazito nacho kinapokea wagonjwa kati ya 20 hadi 35 kwa siku wenye uhitaji wa dharura mbalimbali.