BIASHARA MASAA 24 KUELEKEA MKUTANO WA WAKUU WA NCHI ZA AFRIKA KUHUSU NISHATI



MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema maandalizi ya kuwapokea viongozi mbalimbali wa nchi za Afrika wakiwemo Marais, yanaendelea vizuri, huku biashara zitafanyika kwa masaa 24 kuwezesha wageni kupata huduma mbalimbali wakati wote wa mkutano huo.

Pia, ameagiza ifikakapo Januari 20, kuondolewa kwa malori  yanayoegeshwa ndani ya hifadhi ya barabara kuweka mwonekano wa jiji hilo katika hali ya usafi.

Mkutano huo unaojulikanao 'Mission 300 Afrika Energy Summit', utafanyika Januari 27 na 28, nchini ukijumuisha watu 1500, ukilenga kujadili namna ya kufikisha nishati ya umeme kwa wananchi wa Afrika zaidi ya milioni 300 wakiwemo wa Tanzania.

Chalamila amesema hayo, jijini Dar es Salaam, alipokuwa akikagua maeneo mbalimbali ya mkoa huo yatakayotumika katika mkutano huo, ikiwemo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), barabara na Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mkutano huo.

"Wananchi wote wa Jiji la Dar es Salaam, ambao wanafanya biashara, sasa ni wakati wa kufanya biashara masaa 24, kwani ugeni unakuja ni mkubwa kutoka zaidi ya nchi 30, watahitaji kula chakula, kulala, hivyo wakihitaji huduma mbalimbali wazipate kwa wakati," amesema.

Ameeleza a kuwa, hilo litasaidia kuendelea kuwajengea uwezo na kupata uzoefu kuelekea uzinduzi rasmi wa kuanza biashara masaa 24 kufahamu sehemu yenye changamoto.

Chalamila alisema kwasasa katika Jiji la Dar es Salaam, ziko shughuli zinafanyika kwa masaa 24, ikiwemo usafirishaji, hivyo biashara ziendelee kufanyika muda wote kuelekea katika mkutano huo wa kimataifa, ambapi mwisho wa mwezi watazindua rasmi.