Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imepokea msaada wa mashine tatu za kisasa za uchunguzi na tiba kwa wagonjwa wenye changamoto mbalimbali za macho kutoka Shule ya Kwaya ya Watoto Westminster ya nchini Uingereza (Westminster Cathedral Choir School) kupitia Hospitali ya Mtakatifu Thomas ya nchini humo zenye thamani ya Sh. milioni 325.
Msaada huo unajumuisha mashine ya kutoa tiba ya mionzi kwa muda mfupi ili kuzuia upofu wangojwa wenye shida ya pazia la kuona kutokana na mishipa ya macho kuota au kujaa maji kwenye pazia hilo, mashine ya pili itasaidia wagonjwa waliofanyiwa upasuaji mtoto wa jicho na ikitokea wamepata ukungu utaondolewa ukungu huo kutumia mashine hiyo bila kuhitaji kurudi chumba cha upasuaji na mashine ya tatu ni ultrasound ya macho inayohamishika kwenda alipo mgonjwa hata kama ni chumba cha upasuaji ili kutoa majibu ya wakati huohuo (real time) na kumwezesha mtoa huduma kutoa uamuzi sahihi wa tiba.
Akipokea msaada huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Dkt. Rachel Mhaville ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji amesema, Shule ya Kwaya ya Watoto Westminster ya nchini Uingereza kupitia Hospitali ya Mtakatifu Thomas wamekua na ushirikiano na MNH kwa zaidi ya miaka 17 wa kutoa mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uwezo watoa huduma za uchunguzi na upasuaji wa macho na kuleta vifaa tiba ili kusaidia jitihada za Serikali za kuboresha upatikanaji huduma bora kwa wananchi wake.
Naye Bingwa na Mshauri Mwelekezi wa Macho Dkt. Moin Mohamed kutoka Hospitali ya Mtakatifu Thomas amesema uhusiano uliopo kati yao na MNH ulilenga kutoa mafunzo kwa watoa huduma, kutoa vifaa tiba ili kuendeleza upatikanaji wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi za macho hospitalini hapo na kuongeza kuwa msaada wa mashine hizo utasaidia watanzania wengi wasipoteze uwezo wa kuona.
Naye Bingwa wa Upasuaji Macho Dkt. Joachim Kilemile wa MNH ameushukuru Uongozi wa MNH kuendeleza ushirikiano huo na kumshukuru Dkt. Moin Mohamed ambaye amekuwa hospitalini hapo zaidi ya siku tano akiwajengea uwezo wa namna bora ya kutumia mashine hizo na kuongeza kuwa wananchi wengi watahudumiwa kwa muda mfupi na kwa gharama nafuu.