MKUU wa Kikosi Cha Usalama Barabarani, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi, (SACP) William Mkonda, ametoa onyo kwa madereva wasio zingatia sheria barabarani na hatamvumilia yeyote anayevunja sheria na kusababisha ajali kwa uzembe.
Pia, amesema wameendelea kufanya ukaguzi wa magari ya shule kipindi hiki cha mwanzo wa mwaka wanafunzi wanapofungua shule, huku akisema hawatafumbia macho madereva wote wanaokiuka misingi ya maadili ikiwemo kufanya vitendo vya ubakaji kwa wanafunzi.
Ameyasema hayo Dar es Salaam, wakati akizungumzia mafanikio ya uimarishaji doria kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka na mikakati yao ya kudhibiti ajali kipindi hiki cha mwanzo wa mwaka ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa waliyoyatoa hivi karibuni.
Amesema katika katika oparesheni waliyofanya kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka, walikamata madereva 50 na kuwasitishia leseni kwa muda hususan waliokamatwa kwa ulevi na maegesho yasiyo sahihi.
"Tumejipanga vyema, hatutakuwa na muhari kwa madereva wote wanaokiuka sheria barabarani na kusababisha ajali na vifo vya watu wasio na hatia barabarani, hatuta kuwa na huruma nao, tutawachukulia hatua kali za kisheria.
"Oparesheni tunaendelea nazo tangu mwezi Novemba, tunaendelea kusafisha na kuimarisha doria, opareshani hii itaendelea mwaka mzima, tumejipanga vyema kuhakikisha tunapunguza idadi ajali za barabarani kwa kiasi kikubwa," amesema.
Amesema madereva waliokamatwa wamechukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kusitisha leseni kwa madereva 50, na kuwachukulia hatua za kisheria ikiwemo kuwafikia mahakamani.