MPOGOLO AING'ARISHA ILALA KWA USAFI MAPOKEZI YA WAKUU WA NCHI ZA AFRIKA



Na MWANDISHI WETU

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, leo ameongoza zoezi la kufanya usafi kuanzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) hadi Ufukwe wa Dengu, Kata ya Kivukoni huku akisisitiza wananchi hususan waendesha pikipiki na bajaji kuendelea kuheshimu maelekezo na sheria za usalama barabarani wakati wote wa Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika unaofanyika Januari 27 na 28 mwaka huu.

Amesema tayari maelekezo yametolewa kwa bodaboda na bajaji kuhusu maeneo yaliyokatazwa kupita hususan barabara za Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) hadi maeneo ya katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

Mpogolo ameeleza, mkutano wa Nishati Afrika wa Wakuu wa Nchi ni wa kistoria kufanyika hapa nchini na unastahili kupewa heshima kwani utahusisha nchi zote za Bara la Afrika ukichochewa na ajenda ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye ni kinara wa nishati safi Duniani.

Ameeleza wakati wa kipindi cha mkutano huo zipo barabara na maeneo ambayo yatafungwa kupisha wageni hao hivyo ni muhimu hasa kwa waendesha pikipiki, bajaji na wafanyabiashara wadogo kuheshimu maelekezo yanayotolewa.

Aidha Mpogolo amewaelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Charangwa Seleman, kuwaandikia barua wamiliki wote wa majengo yaliyopo kando ya Barabara ya Nyerere kuhakikisha wanafanya usafi katika maeneo yao.

"Tunataka maeneo haya yawe nadhifu. Waandikie barua hizo leo.Maeneo yote ya majengo yao yawe safi,"amesema.