TMA yatabiri Mvua za Masika



MAMLAKA ya Hali ya Hewa (TMA), imetangaza utabiri wa msimu wa mvua za masika hususan0 maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka, ambapo zinazotarajiwa kunyesha kuanzia Machi hadi Mei, mwaka huku.

Akitangaza utabiri huo jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Ladislaus Chang'a amesema mvua hizo zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Machi, mwaka huu maeneo ya ukanda wa ziwa Victoria, Pwani Kaskazini.

Pia, amesema mvua hizo zinatarajiwa kuanza wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Machi, mwaka huu maeneo ya nyanda za juu Kaskazini Mashariki huku ongezeko zaidi likitarajiwa Mwezi Aprili mwaka huu.

"Mvua hizo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani katika maeneo ya ukanda wa Pwani ya Kaskazini ikiwemo Mikoa ya Kaskazini mwa Morogoro, Pwani na visiwa vya Mafia, Pemba na unguja, Dar es Salaam, Tanga, Kagera, Geita, Mwanza na Shinyanga.

"Pia, mvua hizo zinatarajiwa kuwa za Wastani hadi juu ya Wastani katika maeneo mengi ya nyanda za juu Kaskazini Mashariki na Mashariki mwa mikoa ya Mara na Simiyu," amesema.

Katika ukanda wa Nyanda za Juu Kaskazini hususan Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro mvua zinatarajiwa kuwa za Wastani hadi juu ya Wastani ambapo zitaanza wiki ya pili na ya tatu katika mwezi Machi kuisha wiki ya kwanza Mei Mwaka huu.

Pia Dk. Chang'a amesisitiza kuwa sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi kuchukua tahadhari kuepusha athari zinazoweza kutokea kutokana na hali mbaya ya hewa kuambatana mvua nyingi baadhi ya maeneo.