Balozi Mulamula-Maazimio ya mkutano wa SADC na EAC kichocheo cha usalama DRC
Na MWANDISHI WETU
Mwana diplomasia Nguli, Mbunge Balozi Liberata Mulamula amewapongeza Wakuu wa Nchi za SADC na EAC, kwa maazimio mazuri yenye tija ya kuimarisha usalama na amani, Goma, DRC, huku akisifu jitihada za Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kuwa mwenyeji wa Mkutano huo ikiwa ni sehemu ya kuendelea kulipa heshima Taifa.
Ameyasema hayo, wakati akieleza tija ya mkutano huo na matarajio ya maazimio yake katika utatuzi wa Mgogoro wa Goma, DRC.
"Hakika Rais Dk.Samia ametujengea sifa na heshima kwamba Tanzania daima huwa iko mstari wa mbele katika usuluhishi wa migogoro ya Kanda yetu ya Maziwa Makuu kwa mazungumzo ya amani.
Amewapongeza viongozi wote kufikia makubaliano ya pamoja kusitisha mapigano ya Goma haraka, kurudisha mawasiliano na kufungua Airport na kuhakikisha upitishaji wa misaada ya binadamu unafanikiwa.
Balozi Mulamula alisema amefurahishwa na makubaliano kwamba mazungumzo ya amani ya Luanda na Nairobi, yaliyokuwa yanasimamiwa na Rais wa Angola na Rais Mstaafu wa Kenya Uhuru Kenyatta yaendelee lakini yaunganishwe pamoja.
"Hali kadhalika Mkutano huo wa pamoja uliagiza kuwa Kikao cha pamoja cha Mawaziri wa EAC na SADC kifanyike ndani ya siku thelathini kujadiliana kuhusu: Ripoti ya Mkutano wa Pamoja wa CDFs juu ya kusitisha mapigano na kukomesha uhasama.
"Kuwe na utashi wa kisiasa wa kuzuia mzozo kabla haujatokea na kuangalia chanzo chake kuliko kusubiri hadi kunapokuwa na taharuki ya vita au kudolola kwa mahusiano baina ya nchi na nchi na watu wake inayosababisha kuhatarisha hali ya amani na usalama kama tunavyoona huko Goma, Mashariki ya Kati,"alisema.
"Nimefurahishwa kuona viongozi wa Rwanda na DRC wakishiriki mkutano huo licha ya kwamba, Rais Felix Tshisekedi ameshiriki kwa njia ya mtandao,"alisema.
