Elimu imesaidia kupunguza kifafa na kuongeza uelewa kwa jamii
Na MWANDISHI WETU
CHAMA Cha Wataalamu wa kifafa Tanzania (TEA), kimesema jitihada za kuelimisha jamii kuhusu ugonjwa wa kifafa zimesaidia kupunguza idadi ya waathirika wa ugonjwa huo nchini kwa kiasi kikubwa.
Hayo yamesemwa jini Dar es Salaam na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Fahamu, Ubongo, Mishipa na Uti wa Mgongo, Patience Njenje, kwa niaba ya Chama Cha Wataalamu wa Kifafa Tanzania (TEA), kuelekea katika maadhimisho ya siku ya kifafa Duniani Februari 10, mwaka huu.
Alisema kwa jitihada kubwa ambazo zinaendelea kufanyika nchini za kudhibiti ugonjwa huo, utafiti unaonesha kupungua kwa idadi ya waathirika kutoka 70 hadi 20 na 15 kwa kila watu 1000.
Dk.Njenje alisema, kati ya wagonjwa hao, vijana ndiyo waathirika wakubwa wa ugonjwa wa kifafa kwasababu ya ajali za bodaboda wanazozipata.
Alitaja sababu nyingine za ugonjwa huo ni kula nyama ya nguruwe ambayo haijaiva vizuri, wakina mama kujifungua kienyeji nyumbani, hivyo kusababisha mtoto kupata shida katika ubongo wakati wa kuzaliwa, homa za utotoni ambazo huathiri ubongo wa mtoto ambao huwa haujakomaa.
