Benki ya Exim Tanzania imeimarisha dhamira yake ya kukuza na kuendeleza sekta ya utalii Zanzibar kwa kushirikiana na wadau muhimu wa sekta hiyo, wakiwemo Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), ili kuwezesha waendeshaji wa shughuli za utalii kufanya malipo kama ada za kuingia kwenye hifadhi kwa haraka, kwa usalama na kwa urahisi. Mkutano wa Z-Summit 2025, uliofanyika katika Chuo Kikuu cha SUZA, Tunguu, uliwakutanisha wadau wa serikali, wafanyabiashara, na wadau wa sekta ya utalii na ukarimu ili kujadili suluhisho bunifu za kuboresha nafasi ya Zanzibar kama moja ya vivutio bora vya utalii duniani.
Akizungumza
katika hafla hiyo, Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya Exim, Shani Kinswaga,
aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, alisisitiza safari ya benki
hiyo na Z-Summit tangu kuanzishwa kwake, akieleza kuwa huu ni mwaka wa tatu
mfululizo wa udhamini wao katika mkutano huo.
“Mkutano
huu ni jukwaa muhimu la kushirikiana, kubadilishana maarifa na kujadili mikakati
ya kuimarisha zaidi nafasi ya Zanzibar kama moja ya vivutio bora vya utalii
duniani. Uungwaji mkono wa Benki ya Exim unaonesha imani yetu thabiti katika
sekta ya utalii kama kiini cha ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii,” alisema
Kinswaga.
Kinswaga
alielezea juhudi za benki hiyo katika kutumia teknolojia kutoa suluhisho rahisi
za kifedha zinazokidhi mahitaji ya biashara za utalii. Kwa kuongezeka kwa
mahitaji ya miamala ya kidigitali, Benki ya Exim imeanzisha huduma bunifu za
kibenki, zikiwemo kutumia simu, kadi, na mifumo ya malipo mtandaoni, ili
kuhakikisha ufanisi, usalama, na urahisi kwa wafanyabiashara na watalii.
Akizungumzia
ushirikiano wao na TANAPA, Andrew Lyimo, Mkuu wa Kitengo cha Benki ya Rejareja
wa Benki ya Exim, alisema, “Katika Benki ya Exim, tunatambua kuwa ufanisi,
usalama, na urahisi ni muhimu katika sekta ya utalii. Ndiyo maana
tumeshirikiana na wadau kama TANAPA na NCAA kuwezesha malipo yasiyo ya fedha
taslimu kwa huduma mbalimbali, ikiwemo ada za kuingia kwenye hifadhi. Akaunti
ya Waendeshaji wa shughuli za Utalii inajumuisha Kadi ya Exim TANAPA,
iliyoundwa mahsusi kurahisisha miamala katika maeneo yote ya hifadhi nchini
Tanzania.”
Katika
kuthibitisha dhamira yake ya kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha, Benki
ya Exim ilitangaza mpango wake wa kuendelea kupanua huduma zake Zanzibar. Ikiwa
tayari na matawi mawili yanayofanya kazi, benki hiyo ina mpango wa kufungua
matawi katika maeneo mengine ya kimkakati. Hii inaonesha azma ya Benki ya Exim
ya kusogeza huduma za kibenki karibu na biashara, ikiwawezesha kupata suluhisho
za kifedha zinazosaidia maendeleo ya miundombinu, ukuaji wa biashara, na
ufanisi wa uendeshaji.