Dkt.Tulia-CCM imejipanga kushika dola, vijana jitokezeni kugombea

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Spika wa Bunge na Mlezi wa CCM kwa Mikoa ya Kusini na Kaskazini Unguja, Dk. Tulia Ackson, amesema CCM imejipanga kikamilifu kuhakikisha inaendelea kushika dola katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, kwasababu kazi iliyofanywa na Serikali inatosha kutangaza sera za ushindi.

Dkt. Tulia ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na Wanachama wa CCM katika Ukumbi wa CCM Hanyegwamchana, baada ya kuhitimisha ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar, Februari 20, 2025. Ziara hiyo ililenga kukagua miradi mbalimbali ya CCM pamoja na kuwaeleza wananchi kuhusu malengo ya CCM katika mkoa huo.

Dkt. Tulia amewahimiza vijana wa CCM wenye sifa za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kujitokeza kwa wingi, waweze kuonesha uwezo wao na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa. 

Amesisitiza kuwa CCM ina sera shirikishi zinazotoa fursa kwa kila mtu wakiwemo vijana, kushiriki katika Uongozi na maendeleo ya nchi.

“Ndani ya Chama hiki tunaunganishwa na imani yetu. Kipindi cha Uchaguzi si muda wa kunyoosheana vidole au kuoneshana ubaya, bali ni wakati muhimu wa kushikamana ili kupata ushindi wa kishindo. Hiyo ndiyo sera yetu kuu,” amesema.