Global Youth Empowerment Institute kutoa mafunzo kwa vijana 600 Gairo
Na MWANDISHI WETU
Taasisi ya Global Youth Empowerment Institute (GYEI) inatarajia kuandaa kongamano maalumu la mafunzo kwa vijana zaidi ya 600 wa Wilaya ya Gairo, Mkoa wa Morogoro, litakalofanyika tarehe 8 Februari mwaka huu. Mafunzo haya yatajikita katika sekta muhimu za kilimo, ufugaji, teknolojia na ubunifu, zikiwa ni nyenzo kuu za kuwawezesha vijana kujenga mustakabali bora wa kiuchumi.
Akizungumzia maandalizi ya kongamano hilo, Mkurugenzi wa GYEI, Amina Sanga, amesema lengo kuu la mafunzo haya ni kuiunga mkono serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika juhudi zake za kuhamasisha ubunifu na kuongeza fursa za ajira kwa vijana ili kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
"Huu ni mwendelezo wa jitihada za GYEI katika kuwawezesha vijana kwa maarifa na ujuzi wa kisasa ili waweze kuzitumia fursa zilizopo ndani ya jamii zao. Tunataka kuona vijana wakijiajiri, wakianzisha miradi yenye tija, na hatimaye, kuchangia maendeleo ya Taifa," alisema Amina.
Kongamano hili limeandaliwa kwa ushirikiano na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Gairo, ambapo Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Jabiri Makame anatarajiwa kuwa mgeni rasmi. Pia wakufunzi mashuhuri , viongozi nna wadau wa maendeleo watahudhuria ili kushiriki katika kuwawezesha vijana hawa.
"Tunatoa fursa ya kipekee kwa vijana kujifunza moja kwa moja kutoka kwa wataalamu wa sekta mbalimbali. Mafunzo haya yatawapa ujuzi wa elimu ya fedha, ujasiriamali, matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii, pamoja na uongozi na uzalendo, ili kuwaandaa kuwa nguvu kazi yenye mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii na Taifa," aliongeza Amina.
Kwa vijana wa Gairo, hii ni fursa adhimu ya kujifunza, kushirikiana na kujenga mtandao wa maendeleo. GYEI inaendelea kujidhatiti katika kuwainua vijana wa Kitanzania kuelekea kizazi cha "Kijana wa Tofauti", chenye maarifa, ubunifu na uthubutu wa kubadilisha maisha yao na jamii zao.
