RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwaongoza Wakuu wa Nchi za Afrika zaidi ya sita na wawakilishi wa mataifa hayo wakiwemo Mawaziri, katika kilele cha mkutano wa tatu wa G-25 African Coffee Summit.
Mkutano huo unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere( JNICC), Tanzania ni mwenyeji wa mkutano huo wa nchi zinazozalisha Kahawa barani Afrika, zitatoa tamko la pamoja la Dar es Salaam (Dar es Salaam Declaration) lenye kulenga kukuza thamani ya zao la Kahawa kwa kukabiliana na changamoto zinazokabili zao hilo kwa mataifa hayo.
Kutolewa kwa azimio hilo, ni matokeo ya mjadala wa siku ya kwanza ya mkutano uliofanyika jana, ukiwahusisha Mawaziri wa Kilimo wa Mataifa hayo 25 ya Afrika ya nchi zinazolima kahawa, ambapo kwa Tanzania uliongozwa na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe huku akisisitiza Afrika kujiwekea mipango yake yenyewe katika kuzalisha kahawa na sio kupangiwa na mataifa ya ulaya.
Mkutano huo, uliudhuriwa na washiriki zaidi ya 1500, kutoka mataifa ya Afrika, ulijadili kuhusu maendeleo ya kilimo cha kahawa kwa nchi hizo, ikiwa ni jitihada za makusudi za kuchochea uchumi kupitia zao hilo na ajira kwa wananchi.
Tanzania katika uzalishaji wa kahawa umefikia zaidi ya asilia saba huku matarajio na mipango uliopo ni kufika asilimia 15 kufikia mwaka 2030 huku uzalishaji ukiwa ni tani 55,000 ukikusudiwa kufikia 85 kutokana na jitihada kubwa zinazofanywa na serikali.