INEC kuandikisha wapiga kura wapya zaidi ya 600,000 Dar es Salaam
Na Mwandishi Wetu
Wapiga kura wapya 643,420 wanatarajiwa kuandikishwa katika Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mkoani Dar es Salaam, utakaofanyika kwa siku 7, kuanzia Machi 17 hadi 23, mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume hiyo, Kailima Ramadhan katika mkutano wa wadau wa uchaguzi uliofanyika jijini Dar es Salaam.
“Leo tupo hapa Dar es Salaam ikiwa ni maandalizi ya uboreshaji wa Daftari kwenye mkoa huu, ambapo zoezi litafanyika kwa muda wa siku saba kuanzia tarehe 17 Machi, 2025 na kukamilika tarehe 23 Machi, 2025 na vituo vitakuwa vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni,” amesema Jaji Mwambegele.
Amesema Mkoa wa Dar es Salaam ndiyo wa mwisho katika awamu ya kwanza ya uboreshaji wa Daftari, ilizinduliwa mwezi Julai, 2024 mkoani Kigoma ambapo mpaka sasa zoezi hilo limeshafanyika katika mikoa 28 na mikoa ya Morogoro na Tanga inatarajiwa kukamilisha zoezi hilo tarehe 07 Machi, 2025.
“Hadi leo tarehe 05 Machi, 2025 Tume imeshakamilisha uboreshaji wa Daftari katika Mikoa 28. Kwa mujibu wa ratiba, kwa sasa Tume imeanza maandalizi ya mzunguko wa 13 ambao ni mzunguko wa mwisho wa uboreshaji wa Daftari. Mzunguko huu unahusisha Mkoa wa Dar es Salaam pekee", amesema
"Aidha, uboreshaji wa daftari katika Mkoa wa Morogoro na sehemu ya Mkoa wa Tanga katika Halmashauri za Wilaya ya Bumbuli, Handeni, Pangani na Mkinga unaendelea tangu tarehe 01 Machi, 2025 na utakamilika tarehe 07 Machi, 2025,” amesema Jaji Mwambegele.
Akiwasilisha mada katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Kailima Ramadhan, amesema kwa Mkoa wa Dar es Salaam tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 643,420 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 18.7 ya wapiga kura 3,427,917 waliopo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
“Tume inatarajia baada ya uandikishaji Mkoa wa Dar es Salaam utakuwa na wapiga kura 4,071,337. Aidha, idadi hii inaweza kuongezeka kwa kuwa inawezekana wapo watanzania ambao walikuwa na sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura wakati wa uboreshaji wa Daftari mwaka 2019/20, lakini kwa sababu moja au nyingine hawakuweza kujiandikisha,” amesema Kailima.
Ameongeza kuwa mkoa wa Dar es Salaam una vituo 1,757 vitakavyotumika kwenye uboreshaji kwa mwaka huu ikiwa ni ongezeko la vituo 96 katika vituo 1,661 vilivyotumika kwenye uboreshaji mwaka 2019/20.
Kailima amesema zoezi la uboreshaji wa Daftari linahusu kuandikisha wapiga kura wapya ambao ni raia wa Tanzania wenye umri wa miaka 18 na zaidi na watakaotimiza umri huo ifikapo tarehe ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, kutoa kadi mpya kwa wapiga kura waliopoteza kadi au kadi zao kuharibika na kutoa fursa kwa wapiga kura walioandikishwa kurekebisha taarifa zao yakiwemo majina na taarifa nyingine.
“Uboreshaji wa Daftari pia utahusu kutoa fursa kwa wapiga kura waliopo kwenye Daftari na ambao wamehama, waweze kuhamisha taarifa zao kutoka kata au jimbo walipoandikishwa awali na kuondoa wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo kwenye Daftari kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuukana uraia wa Tanzania na kifo,” amesema Kailima.
