Puma Energy Tanzania Yazindua Awamu ya Pili ya Kampeni ya Usalama Barabarani kwa Wanafunzi wa Shule za Msingi
Na MWANDISHI WETU
Kampuni ya Puma Energy kwa kushirikiana na Shirika la Amend Tanzania, imezindua awamu ya pili ya kampeni ya Usalama Barabarani ya ‘Be Road Safe Africa'.
Kampeni hiyo inalenga kuleta mageuzi kwa usalama barabarani na kuwawezesha watoto na kuboresha uelewa wa usalama barabarani katika jamii zao.
Akizungumza katika ufunguzi huo, jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), William Mkonda, amesema dhamira ya serikali ni kupunguza ajali za barabarani zinazosababisha vifo vya maelfu ya watu kila mwaka.
Amesema ajali za barabarani zimeendelea kuwa changamoto kubwa ambapo kampeni ya ‘Be Road Safe Africa’ inaenda sambamba na jitihada zinazoendelea za serikali katika kuhimiza shughuli za usalama barabarani.
“Takwimu za Jeshi la Polisi zinaonyesha mwaka 2024 pekee, nchi ilirekodi ajali 1,735 za barabarani ambapo ajali 1,198 kati ya hizo zilisababisha vifo vya Watu 1,715, makosa ya kibinadamu, ikiwemo kupuuzia alama za barabarani, kuendesha gari kwa uzembe na mwendokasi, vilichangia 97% ya matukio haya", amesema.
Mkonda amesema wanahimiza sekta binafsi na wadau wa usalama barabarani kuendelea kushirikiana na serikali kuelimisha na kuongeza uelewa kuhusu usalama barabarani.
Pia Mkonda ameipongeza Kampuni ya Puma Energy Tanzania kwa jitihada zake za kutoa elimu ya usalama barabarani.
"Watoto wanaosoma shule zilizo karibu na barabara wako hatarini zaidi, tunashukuru mpango huu na tutaendelea kushirikiana na Puma Energy ili kupanua wigo wa kampeni hii kote nchini", amesema.
Pia Mkonda ametoa wito kwa kampuni zingine kuungana, kuhamasisha usalama barabarani, mafanikio ya biashara zao yanategemea afya na ustawi wa jamii wanazozihudumia.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Uendeshaji wa Puma Energy Tanzania, Mhandisi Lameck Hiliyai, amesisitiza dhamira ya kampuni hiyo katika kulinda usalama na ustawi wa jamii.
“Kwetu Puma Energy, usalama ndiyo msingi wa uendeshaji wa shughuli zetu, kupitia mpango huu, tunatekeleza adhma yetu ya kuzingatia na kusimamia misingi ya afya, usalama, ulinzi na mazingira (HSSE) kuhakiksha watoto, ambao ndiyo kundi hatarishi zaidi la watumiaji wa barabara, wanawezeshwa na elimu ya kuwa salama", amesema.
Hiliyai amesema kampeni ya ‘Be Road Safe Africa’ inaboresha usalama wa watoto wa shule za msingi kupitia programu za elimu zinazowawezesha kuwa watumiaji wa barabara wanaowajibika.
Amesema kupitia shughuli wanazozifurahia na kuzipenda, wanawafundisha watoto kuhusu usalama barabarani na kuwahimiza kueneza ujumbe katika jamii zao.
Hiliyai amesema mojawapo ya shughuli ya kuvutia zaidi katika programu hii 'Mahakama ya Watoto', ambapo watoto huchukua jukumu la 'majaji wa usalama barabarani' na kusaidia kuwawajibisha madereva kwa matendo yao ya barabarani.
Awamu ya pili itaendeleza jitihada zake katika shule za msingi zingine tano ambazo ni Kisukuru (Tabata), Kunguru (Goba), Mjimpya (Kurasini), Ufukoni (Kigamboni), and Salasala (Salasala).
Puma Energy Tanzania inashirikiana na shirika lisilo la kiserikali la Amend Tanzania na washirika wengine wa ndani wakiwemo mabaraza ya usalama na polisi kufanikisha kampeni hii.
