Nchimbi atoa wito Uchaguzi Mkuu 2025
Na CCM
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi amesema msingi wa sera za Chama utabaki kuwa ni maendeleo ya watu, amani na utulivu wa nchi.
Nchimbi ameyasema hayo Aprili 6, 2025, alipokuwa akizungumza na mamia ya wananchi wa mji wa Songea, Liziboni katika Uwanja wa Majimaji na Mshangano.
Katika eneo la Liziboni, Nchimbi alilazimika kusimamisha msafara wake kuzungumza na wananchi waliomsimamisha njiani akitokea Nyasa. Alitumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi wa Songea kwa mchango wao mkubwa uliomuwezesha kufahamika kitaifa na kimataifa.
Katika Uwanja wa Majimaji, alihutubia umati mkubwa wa wananchi waliokuwa wakimsubiri wakati alipofika kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la ghorofa lenye fremu 50 za CCM Mkoa wa Ruvuma. Katika hotuba yake, aliwaomba wananchi wa Songea, mkoa mzima na nchi nzima kwa ujumla kujiandaa kushiriki kwa wingi Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, 2025.
Akiwa Mshangano, ambako alizindua rasmi fremu 50 za tawi la CCM la eneo hilo, Balozi Nchimbi alisisitiza tena umuhimu wa ushiriki mkubwa wa wananchi katika uchaguzi mkuu, akieleza kuwa ni kwa njia hiyo ndipo maendeleo na ustawi wa taifa yanaweza kufikiwa kwa kasi na kwa manufaa ya wote.
Ziara ya Katibu Mkuu huyo ilionesha mapokezi makubwa ya wananchi na kiu ya kusikia mwelekeo wa chama chao kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
