JANETH MAHAWANGA AMPONGEZA RAIS DK.SAMIA KUFANIKISHA DIRA YA MAENDELEO TAIFA YA 2025/2050
KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mtia nia wa ubunge wa viti maalumu Mkoa wa Dar es Salaam, Janeth Mahawanga amepongeza kwa dhati juhudi za serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukamilisha Dira ya Taifa ya maendeleo 2025/2050, hatua inayoashiria dhamira ya dhati ya kuleta maendeleo jumuishi na ushidani kwa Taifa letu.
Mahawanga ameyasema hayo, alipozungumza kukamilika kwa dira itakayoziduliwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan huku akisema ni ushahidi wa uongozi dhabiti, mipango madhubuti na maono ya muda mrefu yenye lengo la kuboresha maisha ya watanzania kwa misingi ya usawa , haki na fursa kwa wote.
Dira ya Taifa ya maendeleo 2025/2050 ina lengo la kuifikisha Tanzania katika maendeleo ya kweli, jumuishi na endelevu kwani imejikita katika kujenga jamii yenye maendeleo ya watu wake kwa ujumla, kupitia mifumo madhubuti ya Uchumi, Siasa, Haki, Diplomasia na Utawala bora.
Kuhusu uchumi, alisema Dira hiyo inatija kubwa katika kuchochea uchumi wa Taifa kwa kuweka msingi wa kuimarisha sekta muhimu kama kilimo, viwanda, madini, nishati na huduma na mwelekeo wa uchumi wa viwanda unaowezesha uzalishaji wa bidhaa zenye kuongezewa thamani hapa nchini hivyo kusaidia kuongeza ajira, kukuza pato la taifa na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje.
Aidha kupitia agenda ya uchumi shindani na jumuishi, dira hii imelenga kuleta usawa wa fursa kwa wananchi wote hasa Wanawake, Vijana na Watu wenye mahitaji maalum katika kunufaika na fursa za kiuchumi.
Katika diplomasia, alisema katika nyanja ya diplomasia, dira imeweka msingi wa kuiwezesha Tanzania kushiriki kikamilifu katika majukwaa ya kimataifa, kuimarisha uhusiano wa kiplomasia, na kuvutia uwekezaji kutoka nje.
Alisema ushirikiano wa kimataifa unaochochewa na dira unatoa nafasi kwa nchi kuimarisha biashara ya nje, kubadilishana teknolojia na maarifa, kushiriki katika suluhishi la changamoto za kikanda na kimataifa.Mifumo ya Haki na Utawala Bora:Dira inatambua umuhimu wa kuwa na mifumo madhuburi ya haki, sheria na utawala bora.
Alieleza kuwa, kuhakikisha kwamba haki zinapatikana kwa wakati na kwa usawa, wananchi wanajengewa imani kwa taasisi za umma na kuchochea mshikamano wa kijamii.
