NIMEFURAHISHWA DIPLOMASIA KUPEWA UMUHIMU DIRA YA MAENDELEO YA TAIFA - BALOZI MULAMULA
Balozi Liberata Mulamula, ambaye ni mtia nia wa ubunge wa viti maalumu nafasi ya vyuo na vyuo vikuu kupitia CCM, amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake mahiri uliowezesha kukamilika kwa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025/50.
Akizungumzia uzinduzi wa Dira hiyo, amesema imekuwa shirikishi na inafurahisha kuwa Msingi wa Dira hiyo ni maendeleo ya watu yanayochochewa na uchumi imara, wenye ushindani na kipato cha juu, kuinua viwango vya maisha ya wananchi na kuondoa umasikini ifikapo 2050.
"Nimefurahishwa kuona Diplomasia imepewa umuhimu katika malengo ya kujenga Tanzania ambayo itakuwa nchi ya mfano ifikapo 2050 katika ustahimilivu, ubunifu, ustawi wa diplomasia barani Afrika na duniani.
"Nimefarijika kuona Dira imetambua mchango mkubwa wa wanawake na vijana kama sehemu ya nguvu kazi ambayo itajengwa katika misingi ya ubunifu, ujasiriamali na uwajibikaji. Kwa kutambua kwamba wanawake na vijana ni sehemu kubwa ya idadi ya watu na ni nguzo muhimu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi," alisema.
Alisema Dira 2050 inaweka kipaumbele wa ushiriki wa makundi haya katika maendeleo, kwa kutumia vipaji, uwezo na hari yao katika kufanikisha ukuaji wa kiuchumi na maendeleo jumuishi.
Alieleza, jambo la Muhimu zaidi, ni Dira 2050 inalenga kuiwezesha Tanzania kutumia rasilimali zake kikamilifu kujitegemea na kujenga uchumi imara na kuwa kitovu cha viwanda katika ukanda wa mashariki na kusini mwa Afrika, ikiwa na uchumi jumuishi na shindani.
"Kwa ujumla Dira hii inaleta matumaini makubwa katika kujenga ‘Taifa Jumuishi Lenye Ustawi, Haki na Linalojitegemea’ kama msingi mkuu wa Dira hii" alisema.
