Kampuni ya iTrust Finance yazindua Mfuko wa Uwekezaji wa Dollar
Na MWANDISHI WETU
Kampuni ya iTrust Finance Limited imezindua rasmi mfuko wa uwekezaji wa pamoja wa iDollar Fund utakao wezesha Watanzania kuwekeza sarafu za kigeni ikiwemo dola na zinginezo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mfuko huo, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa iTrust Finance Limited, Profesa Mohamed Warsame, amesema mfuko huo, unamalengo ya kutoa suluhisho kwa Watanzania wengi ambao tayari wana akaunti za dola katika benki mbalimbali, lakini hukosa njia rasmi na faida kubwa za kuwekeza.
Amesema uwepo wa mfuko huo ni suluhisho kwasababu ya mabadiliko ya sheria ya nchi, ambapo sasa dola haziruhusiwi kutumika moja kwa moja katika miamala ya ndani ikiwepo malipo ya kodi, ada au upangishaji wa nyumba,” amesema Profesa Warsame.
Warsame amesema kwa hatua hiyo ya kisheria, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeelekeza Watanzania kutotumia fedha za kigeni katika miamala ya ndani, hivyo mfuko huu unakuja kama njia mbadala ya kutumia fedha hizo kwa uwekezaji wenye tija na manufaa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Nicodemus Mkama amesema hatua hiyo ni juhudi za kuimarisha uwekezaji nchini na kuongeza mchango wa fedha za kigeni kwa uchumi wa taifa.
Mkama amesema hatua hiyo ni matokeo ya mazingira bora ya kisera na kisheria yaliyowekwa na serikali kupitia CMSA ili kuwezesha maendeleo ya sekta ya masoko ya mitaji.
“Mfuko huu ni nyenzo muhimu kwa ukusanyaji wa fedha za kigeni, unachangia katika uthabiti wa uchumi na kuimarisha uwezo wa nchi kushughulikia changamoto za kigeni. Pia, mfuko huu utawawezesha Watanzania kuwekeza fedha walizonazo katika akaunti zao za sarafu za kigeni,” amesema CPA Mkama.
