Jessica Mshama: CCM inajali uongozi wa vijana
Na MWANDISHI WETU
Katibu wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi UVCCM TAIFA, Jessica Mshama amesema Chama Cha Mapinduzi kinajali sana uwezo wa Vijana katika uongozi ndiyo maana kinawaamini na kuwapa nafasi za juu za kiuongozi.
Amesema hayo kupitia mahojiano ya Televisheni ya Clouds, alipokuwa akizungumzia kazi nzuri inayofanywa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kuwajali na kuwaandaa vijana katika uongozi.
Jessica ameonesha uthabiti wa CCM katika uongozi wake kwa kutofautisha na vyama vingine kutokana na kuwaamini Vijana katika nafasi mbalimbali za kiuongozi na kwamba ushindi wa CCM haupatikani kwa bahati mbaya kwa sababu kimejenga zaidi kwa Vijana.
Kuhusu suala la Uchaguzi, Jessica Mshama amesema kuwa Viongozi wa Juu wa Jumuiya ya UVCCM wamekuwa wakiratibu Mikutano inayohusisha Ziara zao katika Mikoa mbalimbali kwa ajili ya kuhamasisha Vijana kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali pamoja na kujiandaa kupiga kura ifikapo Oktoba 2025.
Jessica aliyasema hayo wakati wa mahojiano na Watangazi wa Kipindi cha Sentro cha Clouds Tv kilichofanyika Jana 08 Julai, 2025 katika studio za Clouds Tv Jijini Dar es Salaam.
Katibu wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi UVCCM TAIFA Jessica Mshama amesema kuwa Madarasa ya uongozi yanayoendeshwa na Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) yamekuwa chachu ya kuoka Viongozi wapya ambao baadhi yao wamejitokeza kugombea nafasi mbalimbali za kiuongozi.
Jessica amewasisitiza vijana kuendelea kutunza amani ya nchi na kuwaepuka vyama vinavyoleta uchochezi wa uvunjifu wa amani huku akiwataka kujiandaa kupiga kura ifikapo Octoba.
