LATRA YATOA MAAGIZO KWA KAMPUNI ZA TIKETI MTANDAO
Na MWANDISHI WETU
MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), imetoa siku 14 kwa kampuni za mifumo ya tiketi mtandao, kuhakikisha wanakamilisha utaratibu huo, watakaoshindwa hawataruhusiwa kutoa huduma hiyo huku tatu zikiwa zimekidhi vigezo na kupata kibali cha kutoa huduma.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa LATRA, Salum Pazzy, huku akiwasisitiza wasafirishaji kuwatumia watoa huduma wa tiketi mtandao wanaotambulika kuepusha usumbufu unaoweza kujitokeza wakati wa ukaguzi endelevu.
“Hatua hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni za Tiketi Mtandao za LATRA za mwaka 2024, zilizotangazwa katika Gazeti la Serikali Na. 20 la Januari 12, mwaka jana, zimeweka takwa la mifumo ya tiketi mtandao nchini kupata kibali cha Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini,”amesema.
Amesema hadi Juni 30 mwaka huu, kampuni tatu za mifumo ya tiketi mtandao zimekidhi vigezo vya kupata kibali kwa mujibu wa Sheria, Mamlaka imeruhusu kampuni hizo kufanya malipo ya vibali na wakishafanya malipo hayo watakabidhiwa vibali vya kutoa huduma za tiketi mtandao.
Ametaja mifumo hiyo ni Otapp Agency Company Limited, Hashtech Tanzania Limited na Iyishe Company Limited.
Pazzy amesema kampuni sita za mifumo ya tiketi mtandao zimeonesha muelekeo mzuri, zinachangamoto ndogo, akizitaja kuwa ni AB Courier Express Limited, Busbora Company Limited Logix Company Limited, Mkombozi Infotech Company, Sepatech Company Limited na Web Corporation Limited.
Ameeleza kuwa, Kampuni mbili za mifumo ya tiketi mtandao zimebainika kuwa na changamoto kadhaa zinazowafanya kukosa sifa za msingi za kutoa huduma za tiketi mtandao.
Amesema kampuni hizo zinapewa siku saba za matazamio, kuhakikisha wamekamilisha matakwa hayo, wakishindwa hawataruhusiwa kuendelea kutoa tiketi mtandao na wateja wao watashauriwa kuhamia kwa watoa huduma waliokamilisha utaratibu.
Ametaja mifumo hiyo ni Duarani Innovative Company na Itule Company Watoa huduma wote ambao hawapo katika orodha iliyotajwa hawatambuliki na Mamlaka kwa mujibu wa Sheria.
Pazzy amesisitiza kuwa, wanaendelea kutoa elimu kushirikiana na wadau husika kukamilisha matakwa ya kisheria, kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za usafiri, kwa urahisi, zenye kuaminika na zenye ufanisi kwa wasafirishaji, watumia huduma na Serikalim kushirikiana na wamiliki wa mifumo na wataalamu wa mifumo wa Serikali.
