SUZA na Chuo Kikuu cha Osaka kuimarisha ushirikiano wa kihistoria kupitia usainiwaji mikataba CHUO Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA)
Chuo Kikuu cha Osaka (OUsaka) Cha Nchini Japani, vinatarajiwa kusaini mikataba ya ushirikiano hususan katika nyanja ya kukuza lugha zao ikiwemo kiswahili na maeneo mengine ya ushirikiano.
Hatua hiyo ni juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika nyanja za lugha na elimu, ambazo zimefikiwa kupitia mazungumzo ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Profesa Moh’d Makame Haji na Makamu Mkuu Muendeshaji wa Chuo Kikuu cha Osaka (OUsaka), Profesa Takemura Keiko.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika jijini Osaka, Profesa Haji alieleza shukrani kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa kuidhinisha na kubariki mchakato wa ushirikiano huo.
Alisisitiza kuwa SUZA inaendelea kutekeleza mkakati madhubuti wa kuunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na taifa kwa ujumla katika kukuza na kutangaza lugha ya Kiswahili duniani, hatua ambayo itaongeza hadhi ya Kiswahili kama lugha ya mawasiliano ya kitaifa na kimataifa.“SUZA ina uzoefu mpana katika kufundisha Kiswahili, kuanzia ngazi ya Shahada ya Kwanza hadi Uzamivu, pamoja na utaalamu maalum katika fasihi, isimu, na tafsiri,” alisema Prof. Haji.
Aliongeza kuwa chuo hicho pia kinatoa kozi mahsusi kwa wanafunzi wa kigeni wanaotaka kujifunza Kiswahili kwa malengo ya kitaaluma au kazi.Kwa upande wake, Prof. Keiko alilipongeza SUZA kwa mchango wake katika kukuza lugha ya Kiswahili na kueleza furaha yake kwa fursa ya kuanzisha ushirikiano na taasisi za elimu ya juu kutoka Afrika Mashariki.
Alieleza matumaini yake kuwa mkataba huo utakuwa msingi wa ushirikiano wenye tija kwa pande zote mbili, hususan kwa OUsaka kujenga uwezo wa kufundisha Kiswahili ndani ya jamii zinazokizungumza na kutoa fursa kwa wanafunzi wake kujifunza utamaduni wa Kiswahili kwa karibu.
Ziara hio iliyomshirikisha Mkuu wa Idara ya Kiswahili kwa Wageni kutoka SUZA, Bi. Fatma Soud na Mkuu wa Huduma za Sheria, Dtk Mtaib Othman ilitoa fursa ya kukutana na wanafunzi wa Japani wanaosoma Kiswahili kwa ngazi ya shahada na uzamili. Uwekaji saini wa mkataba huo umepangwa kufanyika tarehe 7 Julai 2025 katika kilele cha Wiki ya Lugha ya Kiswahili na Utamaduni itakayofanyika Osaka.
Tukio hilo litaashiria mwanzo wa enzi mpya ya ubadilishanaji wa wanafunzi, walimu, na maarifa ya kitaaluma kati ya SUZA na OUsaka, sambamba na kuimarika kwa nafasi ya Kiswahili katika majukwaa ya kimataifa.